Na Judith Mhina - MAELEZO
Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli amerejesha nchi kwa wananchi na
kwamba hayo ni mapinduzi ya ajabu ambayo hayajawahi kutokea katika nchi zetu
hususan Afrika.
Maneno hayo yamesemwa
na Mkurugenzi wa Shirika la Utangazaji la Taifa (TBC) Dkt. Ayub Rioba
alipofanya mahojiano na redio Uhuru mwishoni mwa wiki iliyopita katika ofisi
zao zilizopo Mtaa wa Lumumba jijini Dar-es-salaam.
Dkt.Rioba amesema Mhe.
Rais ameirudisha nchi kwa wananchi kwa kuwa anatekeleza “kile anachoambiwa na
wananchi, na ahadi alizowaahidi wakati akiwaomba kura” anaeleza Dkt. Rioba na
kuongeza kuwa yeye binafsi anamshukuru Mhe. Rais kwa “kuirudishia heshima Tanzania“.
Katika mahojiano
hayo, Dkt. Rioba alieleza kuwa tangu kushika madaraka miaka miwili sasa Rais Magufuli amekuwa ‘busy’ kuhakikisha nchi inakaa sawa kimfumo ndio maana
hajashughulika sana na safari za kwenda nje ya nchi.
Rais anataka
kutengeneza “mfumo wa kimkataba au kibiashara na hawa mabwana wakubwa (wawekezaji
toka nje) utakaowezesha kugawana nusu kwa nusu katika kile kinachopatikana
katika uendelezaji wa rasilimali zetu badala ya mifumo ya zamani ya kukubali
kila mfumo unaoletwa na nchi zilizoendelea” alisema Dkt. Rioba.
Mkurugezi Mkuu huyo
alikieleza kituo hicho cha redio kuwa yeye binafsi anadhani kilichosababisha
Kampuni ya kuchimba Dhahabu ya Barrick kumsikiliza
Mhe Rais ni umakini wa kiongozi huyo kwa “hanunuliki, hahongwi hongwi maana
Afrika ina viongozi wengi ambao wananunuliwa na kuhongwa” lakini sasa wanajua
huyu ni tofauti.
Dkt. Rioba anamuona
Rais Magufuli kuwa kiongozi anayesimamia mambo yanayo wanufaisha wananchi wake na
“hakimbii kimbii kwenda huku na kule kuomba" na kuifananisha nchi yetu na
zile zinazotoa misaada katika nchi nyingine. Kwa kuwa fedha wanazozipata zinatokana
na rasilimali zetu na kueendeleza nchi
zao.
Mhe Magufuli alisema;
“Nchi yetu ilitakiwa kuwa Donor Country,
yaani nchi inayotoa misaada kwa nchi nyingine”.
Ninachoweza kuwaambia
Watanzania wenzangu miaka miwili ya Serikali ya Awamu ya Tano madarakani,
hakika viongozi wetu wameonesha nia nzuri na wanatakiwa kuunga mkono kwa hili
analolifanya Rais Magufuli wakati huu wa mpito.
Nchi yoyote inapopita
katika mpito ni lazima kuna mambo yalikuwa hayaendi sawa na mengine yamekwenda sawa. Mpito ukitokea
kuna mabadiliko yatakayojitokeza. Mfano Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere
alipendekeza mfumo wa vyama vingi japo wananchi wengi, bado waliutaka mfumo wa chama
kimoja. Aidha kutokana na kubadilishana
uongozi hapa Tanzania, mabadiliko mengi yalijitokeza ambayo yalikuwa mazuri na
mengine sio mazuri kwa kuwa ni kipindi cha mpito.
Dkt. Rioba amesema ujio
wa Rais Magufuli ulikuwa ujio muhimu sana kwa wakati huu, kwa ajili ya kurekebisha
yale yote yaliyojitokeza ambayo hayakuwa sawa. Akitoa mfano wa mwana falsafa
mmoja anayeitwa Fans Fanon wakati wa vita vya ukombozi nchini Algeria alisema:
“Kila kizazi
kinakutana na majukumu yake ya msingi ya kutekeleza au kuyatelekeza na kusubiri
matokeo yake”
Mkurugezi Mkuu huyo
wa TBC alieleza kuwa kwa maoni yake Rais Magufuli amekuwa kiongozi sahihi
aliyekuja kwa wakati sahihi, ili kurekebisha mambo kwa namna moja au nyingine ambapo
hapa na pale tulijikwaa kwa sababu tulitoka nje
ya misingi iliyojengwa na Taifa
letu.
Kuhusu suala la kuwa
na uchumi mzuri katika nchi Rioba amesema tafiti zinafanyika kwa mrengo wa
kimagharibi zaidi ambapo, wanahalalisha mifumo ya uchumi wanayoitaka wao. Wachumi
walio wengi wanasema ili uchumi uwe mzuri na nchi kuendelea ni lazima kuwa na Ardhi,
tekinolojia, rasilimali ziwe nyingi nk , lakini sio kweli.
Mfano nchi ya Singapore
hawana rasilimali zaidi ya bahari na samaki lakini uchumi wao ni mzuri sababu
moja kubwa ni uongozi bora ambao unasimamia matumizi sahihi ya rasilimali kwa
manufaa ya wananchi wa nchi husika. Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo ni nchi ya
4 duniani kwa wingi wa madini lakini haijaendelea, mpaka leo kuna watu wanaomiliki
madini katika nchi hiyo wako nje hivyo faida yote inayopatikana kutokana na
madini hayo inazinufaisha nchi za nje.
Jambo la msingi Rais Magufuli
anataka rasilimali zilizopo, hata kama kidogo kitumike kwa manufaa ya wananchi
wanyonge wa Tanzania. Tanzania ya Rais
Magufuli amesema hapana haya madini yanayopatikana hapa Tanzania ni lazima
tugawane nusu kwa nusu.
Dkt. Rioba anasema Rais
ameonesha mfano kwa nchi nyingine za Afrika zenye rasilimali kama zetu, kuwa
hili la kugawana faida nusu kwa nusu, hata kama hatuna tekinolojia na mitaji
linawezekana.
Zipo nchi nyingi za
Afrika ambazo zilitumia rasilimali zao vibaya mfano, Siera Leoni, Liberia
wakawa wanachimba almasi kwa ajili ya kuendesha vita na kununua silaha kutoka
nchi zilizoendelea. Afrika ifike mahali
ioneshe ukomavu na kuacha mambo ya kipumbavu kama hayo ioneshe kuwa Afrika ina
watu wanaweza kufikiri na kuweza kugawana rasilimali kama alivyofanya Rais
Magufuli.
Ukiangalia nchi ya
Nigeria asilimia 80 ya mafuta yanayosafirishwa kwenda nje ni asilimia 1 tu ya
mafuta hayo ndio yanarudi Nigeria, lakini Tanzana ya Magufuli amesema hapana
Akitoa mfano Dkt
Rioba alisema Baba wa Taifa mara baada ya Uhuru wa Tanganyika, wasomi walikuwa
wachache sana wasingeweza kutosheleza katika masuala ya utaalam na kuleta
maendeleo kupitia rasilimali tulizonazo.
leo hii nchi yetu imepiga hatua kubwa sana katika suala la taaluma na
elimu ambapo hatukuwa na Chuo Kikuu hata kimoja. Leo Tanzania ina vyuo vikuu
takriban 50, na wataalamu wako wengi, tunachokosa ni Wataalamu wanaoipenda nchi
yao wazalendo wenye nia ya kusukuma gurudumu la maendeleo.
Dkt. Rioba anaeleza
kuwa ni vizuri kuwa na waaalam vijana wenye moyo wa kujituma na uzalendo na kuwa
tayari kuwa watumishi wa wananchi na kusaidia
kutimiza ndoto ya Tanzania ya viwanda na
ndivyo anavyotaka Rais Magufuli.
Akizungumzia suala la
kuondoa dhana ya kuwa na matabaka ya watu katika Taifa, Rioba amesema kwa sababu Tanzania iko katika
mpito, ambapo ilitoka katika misingi ya Ujamaa na Kujitegemea (Azimio la Arusha)
na sasa ni kama kutengeneza Azimio la Arusha jipya lakini katika muktadha wa
zama za sasa. Kwa wale watanzania ambao ni wazalendo kabisa kabisa, Dkt. Rioba anasema
watakubaliana nae kuwa anayoyafanya Rais Magufuli ni lazima aungwe mkono kwa
kuwa anaipeleka nchi panapostahili.
Dkt. Rioba katika
mahojiano hayo amesema ni wakati sasa kwa kila Mtanzania kuona uchungu kwa kila
aina ya wizi wa rasilimali za nchi na kwamba dhambi kubwa ambayo watanzania
wanaweza kuifanya ni kudhani kuwa jukumu la kulinda rasilimali za nchi ni la Rais
Magufuli pekee.
“Haijawahi tokea
kiongozi yeyote barani Afirika kusema wananchi tumeibiwa mno na mbali zaidi,
kutafuta suluhisho la kuibiwa huko. Hongera Rais Magufuli jitihada zako ni
ukombozi kwa rasilimali zote Barani Afrika na mwisho wa Bara la Afrika kuwa Shamba
la Bibi (akimaanisha kila mtu anakuja kujichukulia na kundoka)” Dkt. Rioba
alimazilia mahojiano hayo.
|
Navigation
Post A Comment: