MBAO FC WANATAKIWA KUBADILIKA

Share it:

Kikosi cha wakata miti MBAO FC Wakiwa katika pozi la picha.
Mechi iliyopita ambayo ilichezwa katika dimba la ccm kirumba jijini mwanza kati ya Mbao fc na Mbeya city.



Nianze kwa kuwasabahi wasomaji wa mtandao wa maduka online bila shaka mpo salama kabisa na mnaendelea na majukumu ya kila siku.na baada ya salamu basi tuelekee katika uchambuzi.

MBAO FC ni kati ya timu 16 zinazoshiriki Ligi kuu ya Tanzania Bara msimu huu wa 2016/2017.

Ni timu yenye makazi yake kanda ya Ziwa Viktoria mkoani Mwanza, ambayo imepanda daraja msimu huu na kuwapa faraja wakazi wa ukanda huo kwa kuwa na timu tatu kwenye ligi hiyo ikiwemo Toto African nayo ya Mwanza na Kagera Sugar ya mjini Bukoba.


Rekodi ya timu hii kwenye mechi zake tatu ilizocheza tangu kuanza kwa ligi msimu huu si nzuri, kwa sababu imetoa suluhu tasa mechi moja ugenini kwa Stand United, ikafungwa jumla ya magoli matano na Mwadui FC pamoja na Mbeya City tena ikiwa nyumbani.

Mechi kati yake na Mwadui ilifungwa 1-0 kisha ikachezea goli 4-1 mbele ya Mbeya City ambao ni watoto wa halmashauri ya Jiji la Mbeya, mechi hizi zote Mbao alikuwa kwenye uwanja wa nyumbani.

Kiuhalisia vipigo hivi viwili ndivyo vilianzisha minong'ono kwa wapenzi wa soka hapa nchini, kuwa haikujiandaa na kwamba ilipanda daraja kwa mizengwe jambo ambalo binafsi siungi mkono.

Ninazungumza hivi kwa sababu mechi tatu ni chache mno kuwahukumu kama wanavyowahukumu baadhi ya wadau wa soka ambao wamefikia kiwango cha kusema Mbao haitaweza kubaki ligi kuu kwa mwendo huo.

Kama inavyofahamika mpira ni dakika tisini, kesho kutwa Mbao watakuwa wageni wa African Lyon, halitakuwa jambo la ajabu wakishinda mechi hiyo kwa magoli ambayo watu hawataamini, ndivyo mpira ulivyo.

Kuwanyooshea kidole wachezaji na uongozi mzima wa timu hiyo changa kwenye ligi hii yenye kila aina ya mikiki mikiki ni kawavunja moyo, kitu ambacho si kizuri kwa wakati huu.

Tunatakiwa kuwapa moyo kuwa wataweza kufanya mapinduzi ya soka kwenye ligi kuu ya msimu huu kwa kushika hata nafasi nne za juu katika msimamo mwisho wa ligi.

Timu kubwa duniani ikiwemo Manchester United ya Uingereza katika msimu wa 2007/2008 walianza kwa mtindo huu walioanza nao Mbao FC, walitoa suluhu mbili kwa Reading na Portsmouth  kabla ya kufungwa mechi mbili na Bolton Wanderers na Arsenal.

Mwisho wa msimu, timu hiyo ilitwaa ubingwa wa ligi, ikatwaa kombe la Ulaya (UEFA) na ngao ya hisani; hivyo hakuna linaloshindikana kwenye mpira, kila mwanamichezo analijua hili.
Hivyo natoa rai tuziunge mkono timu changa kwenye ligi kwa kuzipa moyo ili tuone ligi yenye ushindani tofauti na mazoea ya kuwa zipo timu kwenye ligi ambazo hupanda kwa lengo la kugawa pointi tatu kwenye kila mechi kwa timu kongwe.


Imeandaliwa na Chechambo William wakishilikiana na Joel Maduka.

Share it:

michezo

Post A Comment: