Kamanda wa polisi mkoa wa Shinyanga ACP Muliro Jumanne Muliro |
Matukio ya watu kuchukua maamuzi ya kujiua katika manispaa ya Shinyanga yanazidi kushika kasi leo Jumapili June 18,2017 majira ya saa 10 alfajiri kijana aitwaye Paulo Ezekiel (17) mkazi wa mtaa wa Mazinge kata ya Ndembezi aliyekuwa anafanya kazi ya kuendesha baiskeli maarufu 'daladala 'amefariki dunia kwa kujinyonga kwa kamba juu ya mti jirani na nyumba yao.
Inaelezwa kuwa huenda ni ugumu wa maisha ndiyo umechangia kifo cha kijana huyo kwani enzi za uhai wake alikuwa analalamika kuwa maisha ni magumu.
Akielezea kuhusu tukio hilo. baba mzazi wa marehemu Ezekiel Paulo, alisema kijana wake huyo hapo awali alikuwa na ugomvi na marafiki zake waendesha baiskeli maarufu daladala, ambapo ugomvi huo ulisuluhishwa akaendelea na majukumu yake.
Alisema chanzo cha kifo kijana wake bado hajakifahamu vizuri, ingawa kijana wake huyo pamoja na kujishughulisha na shughuli mbalimbali za kujipatia kipato ikiwemo kuendesha baiskeli 'daladala' alikuwa akilalamika mara kwa mara kuwa maisha ni magumu.
“Ilipofika majira ya saa 10 usiku nilisikia mlango wa chumba cha kijana wangu ukifunguliwa, nikajua ametoka kwenda kujisaidia lakini ukapita muda mrefu sikusikia kuwa amerudi, ndipo nikatoka nje na kukuta hadi geti la uwani likiwa wazi, nikaanza kumtafuta bila mafanikio,”alieleza baba yake mzazi.
“Niliporudi ndani nikamwamusha mama yake mzazi na wadogo zake wawili wa kike, tukaanza kumsaka ndipo tukamuona akiwa juu ya mti jirani na nyumba yetu, akiwa ameshafariki tayari kwa kujinyonga na kamba”,aliongeza.
Kamanda wa jeshi la polisi mkoani Shinyanga Jumanne Murilo amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na hakuna mtu yeyote anayeshikiliwa na jeshi juu ya kifo hicho.
Matukio ya watu kuchukua uamuzi wa kujiua yameanza kukithiri katika manispaa ya Shinyanga ambapo ndani ya mwezi mmoja huu wa Juni hili ni tukio la nne.
Tukio la kwanza ni la Luhende Lusangija (34) mkazi wa kata ya Ngokolo aliyejiua kwa kamba,la pili ni la Mwenyekiti wa waendesha bodaboda katika manispaa ya Shinyanga Jacob Paul mkazi wa kata ya Ngokolo aliyejiua kwa waya wa simu la tatu ni la Saada Elias mkazi wa kata ya Ndembezi aliyekatisha maisha yake kwa kujichinja kwa kisu na chupa ya soda.
Na Kadama Malunde-Malunde1 blog
Post A Comment: