Waziri
wa Maji na Umwagiliaji, Mhandisi Isack Kamwelwe(katikati) akiwa katika picha ya
pamoja na viongozi wa Mkoa wa Simiyu na wadau wa Mradi wa kukabiliana na
changamoto zitokanazo na Mabadiliko ya Tabianchi unaotekelezwa Mkoani humo mara baada ya
ufunguzi wa kikao cha wadau hao kilichofanyika Mjini Bariadi.
Na Stella Kalinga, Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Simiyu
Serikali ya Tanzania kwa
kushirikiana na Serikali ya Ujerumani, Mfuko wa Mabadiliko tabia nchi
(CGF) na wananchi, imetenga kiasi cha shilingi bilioni 375.4 kutekeleza
Mradi wa kukabiliana na changamoto zinazotokana na mabadiliko ya tabia
nchi mkoani SIMIYU kwa awamu ya kwanza, ambao
utakuwa suluhisho la kudumu la tatizo la maji mkoani humo.
Hayo yamesemwa na Waziri wa Maji na
Umwagiliaji Mhandisi Isack Kamwelwe wakati akifungua kikao cha wadau wa
mabadiliko ya tabia nchi kilichofanyika Mjini Bariadi Mkoani Simiyu.
Waziri Kamwelwe amesema
moja ya shughuli muhimu na kubwa katika utekelezaji wa Mradi wa kukabiliana na
changamoto zinazotokana na mabadiliko ya tabia nchi, ni ufikishaji wa huduma ya Maji ya Ziwa
Victoria katika Mji wa Bariadi , Busega na Itilima kwa awamu ya kwanza na
baadaye katika Wilaya ya Meatu na Maswa.
Ameongeza kuwa upatikanaji
wa maji katika Mkoa wa Simiyu uko chini ikilinganishwa na wastani wa Kitaifa na
kwa kutambua hali hii, Serikali kwa
kushirikiana na wadau wa maendeleo ilibuni mradi hu, ili kupata suluhisho la kudumu la tatizo la maji kwa wananchi na mifugo
ambayo ni moja ya shughuli za kiuchumi za wananchi wa Mkoa wa Simiyu.
Aidha, Waziri Kamwelwe
amesema lengo la mradi huu ni kuboresha Afya na kuongeza uzalishaji maji ili
kuinua hali ya maisha kwa wananchi walioathirika na mabadiliko ya tabia nchi,
ambapo amebainisha kuwa katika kufikia lengo shughuli mbalimbali zitatekelezwa
katika nyanja za maji safi na usafi wa mazingira, kilimo endelevu na ufugaji.
Waziri pia amebainisha
kuwa kutakuwa na ujenzi wa mabwawa ya kilimo cha umwagiliaji endelevu na maji
ya mifugo, ujenzi wa mabwawa ya kutibu maji taka, vyoo vya mfano katika Shule
na Vituo vya Afya.
Kwa upande wake Mkuu
wa Mkoa wa Simiyu Anthony Mtaka ameishukuru Serikali kwa kutekeleza mradi huo
ambao utawasaidia wananchi wa mkoa huo na utakuwa chachu katika Ujenzi wa
Viwanda mkoani humo kwa kuwezesha upatikanaji wa maji ya uhakika.
“Wananchi wa Mkoa wa
Simiyu wote wanausubiri sana mradi huu wa maji ya Ziwa Victoria; pia Mkoa wetu
unaenda kwenye uwekezaji wa viwanda vikubwa na changamoto tuliyonayo ni suala la
upatikanaji wa maji ya uhakika, utekelezaji wa mradi huu utatusaidia sana
katika viwanda” amesema Mtaka.
Katibu Mkuu Wizara ya
Maji na Umwagiliaji Profesa Kitila Mkumbo amesema kuwa Simiyu ni Miongoni mwa Mikoa
yenye kiwango cha chini cha upatikanaji wa huduma ya maji ambayo Serikali imetoa
kiupaumbele cha kuipa fedha kutoka katika Fedha za Mfuko wa Maji ili kutekeleza
miradi ya maji itakayoibuliwa na kuwasilisha maandiko yake wizarani.
Kwa upande wake Katibu
Tawala Mkoa wa Simiyu, Ndg.Jumanne Sagini amewahimiza Wataalam wa Halmashauri
kwa kushirikiana na Mkoa kuandaa maandiko ya kuibua miradi ya Maji itakayowasilishwa
wizara ya maji, kwa lengo la kuomba
fedha za kutekeleza miradi hiyo ili kuongeza
na kuboresha upatikanaji wa huduma za maji mkoani humo.
Mradi wa kukabiliana
na changamoto zinazotokana na mabadiliko ya tabianchi Mkoani SIMIYU ambao
zabuni yake imepangwa kutangazwa Januari 2018; utatekelezwa kwa awamu mbili awamu
ya kwanza utaanza na Mji wa Bariadi, Busega na Itilima pamoja na vijiji 278
vilivyopo pembezoni mwa bomba kuu umbali wa Kilomita 12 kila upande, baadaye maeneo mengine ya Wilaya za Maswa na
Meatu.
|
Post A Comment: