Waziri wa Viwanda, Biashara na
Uwekezaji, Mhe..Charles Mwijage akizungumza na wadau wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji wa Mkoa wa Simiyu wakati wa Ziara yake Mkoani
humo.
|
Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji Mhe. Charles
Mwijage amesema njia nzuri ya kufikia Uchumi wa Kati ifikapo mwaka 2025 ni kupitia
Uchumi wa Viwanda jumuishi.
Waziri Mwijage ameyasema hayo alipozungumza na wadau
wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji wa Mkoa wa Simiyu wakati wa ziara yake Mkoani
humo, ambapo alisisitiza juu ya Ujenzi wa Uchumi wa Viwanda ulio imara,
shindani na endelevu, utakayozingatia mambo muhimu matatu ambayo ni soko,
malighafi na teknolojia.
Amesema lengo la
Serikali ni kuhamasisha ujenzi wa Uchumi wa Viwanda Jumuishi ambao
unawahusisha watu wengi kupitia viwanda vidogo na vya kati,vitakavyotumia
malighafi zitakozozalishwa hapa nchini vilivyopo katika maeneo mbalimbali
nchini, ukiwepo mkoa wa Simiyu ambao
umeonekana kufanya vizuri katika eneo hilo.
“Safari ya Simiyu imeanza vizuri na lengo la safari
ni kuhamasisha Watanzania kujenga uchumi wa viwanda jumuishi, viwanda ambayo
malighafi yake inazalishwa na wananchi
wenyewe, vitatoa ajira kwa wananchi walio wengi, vitatumia malighafi asilia na
kutoa mazao yenye matumizi makubwa” alisema Mwijage.
Waziri Mwijage amepongeza juhudi zinazofanywa na
Mkoa wa Simiyu katika Ujenzi wa Uchumi wa Viwanda kupitia Falsafa ya “Wilaya
Moja Bidhaa Moja Kiwanda Kimoja” ambapo sasa umejipanga kuelekea kwenye “Kijiji
Kimoja Bidhaa Moja”.
Ameongeza kuwa mwaka 2018/2019 Serikali kupitia Shirika
la Kuhudumia Viwanda Vidogo(SIDO) litawasaidia wananchi kupata mafunzo ya
ujasiriamali, uzalishaji na uchakataji, ambapo ameuhakikishia Viongozi wa Mkoa
wa Simiyu kuwa Ujenzi wa Ofisi ya SIDO ya Mkoa huo eneo la Isanga Mjini Bariadi
utakamilika kabla ya kuanza kwa vikao vya Bunge la Bajeti mwaka 2018, kwa kuwa fedha za ujenzi zipo.
Sanjali na hilo Waziri Mwijage amewataka Maafisa
Ushirika kuwahamasisha wananchi kujiunga katika vikundi ili waweze kukopeshwa
mitaji ya kuanzisha viwanda vidogo na Serikali pamoja na Taasisi nyingine za
Kifedha kwa kuwa ni rahisi zaidi vikudi kufikiwa kuliko mtu mmoja mmoja.
Wakati huo huo Mwijage amewataka watendaji wote wa
Serikali kuondoa vikwazo na kuacha urasimu unaoweza kuwakwamisha wawekezaji
katika maeneo mbalimbali hapa nchini ili kuweza kuufikia Uchumi wa kati ifikapo
mwaka 2025.
Akiwasilisha tarifa ya Mkoa, Katibu Tawala Mkoa
Simiyu, Ndg. Jumanne Sagini amesema ili kuandaa mazingira mazuri
yatakayowawezesha wawekezaji kuvutiwa na kuwekeza mkoani humo, wametenga maeneo
ya uwekezaji na madawati ya uwekezaji kwa kila Halmashauri na timu mahsusi ya
Mkoa ya kuanzisha na kuendeleza dhana ya Simiyu ya Viwanda inayoongozwa na
Katibu Tawala Mkoa.
Mwenyekiti wa Wafanyabiashara wa Mkoa wa Simiyu,
Njalu Silanga amesema wako tayari kuunga mkono juhudi za Serikali kwa vitendo
katika Ujenzi wa Viwanda vidogo na vya kati na akaomba Meneja wa SIDO Mkoa atembelee
viwanda vilivyopo ili aweze kutoa ushauri juu kuboresha uendeshaji wa viwanda
hivyo katika tija.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe.Anthony Mtaka
amesema kupitia SIDO mkoa huo unaweza kufikia Uchumi wa Kati. “Tungehitaji kuwa
ni Mkoa ambao value addition(kuongeza thamani) itafanyika kupitia SIDO, mahali
ambapo mtu mwenye milioni tatu wakiungana kikundi cha walima alizeti
wanaprocess(wanachaka) wenyewe mafuta” alisema Mtaka.
Pamoja na kuzungumza na wadau wa Viwanda, Biashara
na Uwekezaji wa Mkoa wa Simiyu, Waziri Mwijage alifungua Jengo la muda la Ofisi
ya SIDO Mkoa wa Simiyu lililopo Mtaa wa Malambo Mjini Bariadi na kukagua eneo
la ujenzi wa Ofisi mpya ya SIDO itakayojengwa na SUMA JKT, ambayo inatarajiwa
kukamilika kabla ya kuanza kwa vikao vya Bunge la Bajeti mwaka 2018.
Post A Comment: