Mbali na mwezi Februari kuwa mfupi, kitu kingine kinachoupa umaarufu mwezi huu ni kujawa na shamrasharma za sikukuu ya wapendanao au ‘Valentine’s Day.’ Sikukuu hii huadhimishwa kila ifikapo Februari 14 ya kila mwaka, ambapo shughuli na matukio mbalimbali ambayo huonyesha ishara ya upendo hutawala.
Umaarufu wa sikukuu hii umeendelea kushika kasi kote duniani kutokana na uzito wa maana halisi ya neno ‘upendo’ ambalo ndilo hutawala miongoni mwa washerehekeaji.
Miongoni mwa matukio maarufu yanayofanyika katika kipindi hiki ni pamoja na watu kuwatumia wapendwa wao kadi zenye jumbe za upendo au mapenzi, kutuma zawadi kama vile maua au chokoleti kwa wapenzi wao, pamoja na kuandaa mitoko kwenye sehemu ambazo zimeandaliwa kwa mandhari ya wapendanao.
Andika ujumbe mfupi. Unaweza ukaandika ujumbe mfupi wa upendo na kisha ukauweka kwenye mkoba au begi la mpendwa wako ambao ataupata pindi akifika kazini. Hakuna jambo zuri kama kuanza shughuli za asubuhi kama kukutana na ujumbe utakaoufanya moyo wako kujisikia vizuri, kupendwa na kuthaminiwa.
Tuma kadi, maua au chakula. Ingawa unaweza kuwa sio utamaduni wa watanzania wengi au dhana hii kuonekana kupitwa na wakati, lakini unaweza ukamtumia mpenzi wako kadi nzuri yenye ujumbe wa mapenzi na maua ya kuvutia, au chakula anachokipenda mpaka mahali alipo.
Mtembelee ofisini mpenzi/mpendwa wako ofisini. Unaweza ukamshangaza mpendwa wako kwa kumtembelea muda wa mchana, ukiwa na chakula anachokipendelea sana.
Panga mtoko kwa kushtukiza. Ili kunogesha siku hii unaweza ukaamua kwenda kwenye hoteli au mgahawa na kuutumia muda wenu vizuri bila ya kumuambia kabla. Inaweza kuwa baada ya kumaliza shughuli zenu za siku nzima.
Endesha gari mkiwa pamoja. Inawezekana kila mtu hutumia gari lake kwenda na kurudi kazini, lakini unaweza kuitumia siku hii kwa kuamua kumpeleka na kumrudisha. Hii itawapatia fursa ya kutumia muda mwingi mkiwa pamoja.
Mjazie mafuta gari lake. Kama huwa haufanyi hivi mara kwa mara basi kipindi hiki unaweza ukamshangaza mpenzi wako kwa kumjazia mafuta gari lake ‘full tank.’
Fanya jambo zuri kwa mama yake, baba, kaka au dada. Unaweza kwenda mbali zaidi kwa kuwafanyia matendo ya upendo ndugu na jamaa wa mpenzi wako. Kama vile kujumuika kwa pamoja kwa chakula, kulipa karo ya shule au hata kuwanunulia kitu ambacho wazazi wake wanakipendelea.
Mpikie chakula cha usiku. Ni mara chache wanaume huingia jikoni kuipikia familia au wapenzi wao. Utumie msimu huu kwa kumshangaza mpenzi wako kwa kupika chakula cha jioni ili naye aonje mapishi yako.
Itumie siku hiyo kwa kuzungumza kuhusiana na mipango ya maisha yenu. Inawezakana huwa mnapata muda mchache wa kuzungumza mustakabali wa maisha yenu au hampati kabisa. Itumie siku hiyo kwa kutulia sehemu tulivu pamoja na kujadili au kutafakari kwa pamoja mwenendo wa maisha yenu.
Mfulie nguo zake, kama huwa hufanyi hivyo. Hakuna shughuli ambayo watu wengi hawaipendi (hususani wanaume) kama kufua. Endapo mpenzi wako huwa anakufulia mara zote, basi mshangaze siku hiyo kwa kumfulia nguo zake.
Itenge siku maalum kwa ajili yake, panga kufanya vitu anavyovipendelea. Kuna vitu vingi ambavyo wapenzi huvifanya ambavyo siyo lazima hupendelewa na wote. Unaweza ukaitenga siku hiyo kwa kufanya vitu ambavyo mpenzi wako anavipendelea sana.
Mchumbie. Inawezekana mmekuwa kwenye mahusiano kwa muda mrefu lakini hamkupata fursa ya kufanya jambo hilo kuwa rasmi. Itumie siku hiyo kumchumbia mpenzi wako na kumjulisha kwamba unataka kuishi naye milele.
Mtambulishe mpenzi wako kwa familia, ndugu, jamaa na rafiki zako. Huchukua muda kidogo mpaka wapenzi wakaamua kutambulishana kwa ndugu zao au watu wa karibu. Kama mmetumia muda wa kutosha na mnapendana kwa dhati, itumieni siku hiyo kutambulishana kwa wazazi, ndugu, jamaa na marafiki.
Post A Comment: