WATANZANIA WATAKIWA KUWA NA UTAMADUNI WA KUVISAIDIA VITUO VYA WATOTO YATIMA.

Share it:

Mgeni rasmi Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Baraza la Taifa la Usalama Barabarani, Mhandisi Hamad Masauni



NAIBU Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Baraza la Taifa la Usalama Barabarani, Mhandisi Hamad Masauni amewaomba Watanzania kuweka utamaduni wa kuvisaidia vituo vya watoto yatima nchini ili kuwasaidia watoto hao ambao wanaishi katika mazingira magumu.

Masauni alisema hayo mara baada ya kukabidhi misaada mbalimbali katika Kituo cha Watoto Yatima cha Moyo wa Huruma ambacho kinasimamiwa na Kanisa Katoliki mjini Geita.

Naibu Waziri huyo ambaye yupo mjini humo kwa ajili ya kuadhimisha Wiki ya Nenda kwa Usalama ambayo aliizindua jana Septemba 26 katika Viwanja vya CCM Kalangalala ambapo inafanyika kitaifa mjini humo.

Masauni aliwaongoza Wajumbe wa Baraza la Taifa kukusanya fedha taslimu shilingi 1,119,000 kituoni hapo ambapo licha ya fedha hizo Baraza hilo lilitoa misaada mbalimbali ikiwemo mchele gunia moja, kilo 50 za sukari, dumu la mafupta ya kupikia, sabuni Katoni 11 pamoja na fulana 100, alisema lazima Watanzania tuweke utamaduni wa kuvichangia vituo vya watoto yatima. 

“Natoa pongezi kwa uongozi wa Kanisa Katoliki kwa kukisimamia kituo hiki, kuishi na watoto wetu, kuwahudumia vizuri, kwa kweli hili linapaswa kupongezwa. Tupo hapa Geita kwa ajili ya kuadhimisha Wiki ya Nenda kwa Usalama Barabarani lakini tumeguswa na kuamua kutoa michango mbalimbali kwa kituo hiki, na tunawataka Watanzania pia waweke utamaduni huu wa kuvisaidia vituo hivi katika sehemu mbalimbali waliopo nchini,” alisema Masauni.

Masauni aliongeza kuwa, Serikali ya Rais John Magufuli ipo kwa ajili ya kuwasaidia Watanzania wote, kama mnavyoona katika elimu imeweka kipaumbele ili watoto wetu waweze kusoma katika mazingira mazuri.

Kwa upande wake Katibu wa Baraza la Taifa la Usalama Barabarani, Naibu Kamishna, Mohamed Mpinga alitoa pongezi kwa Naibu Waziri Masauni kwakuwaongoza kutoa misaada hiyo kwa kituo hicho.

“Mwenyekiti wa Baraza ametuonyesha njia, ametuongoza na kuweza kufanikisha zoezi hili la uchangiaji, tunamshukuru sana kwa uamuzi huo wa busara wenye nia njema ya kuwasaidia watoto wetu.” Alisema Mpinga.

Aidha, Mlezi wa Kituo hicho, Sista Adalbera Mukure alimshukuru Masauni pamoja na Wajumbe hao kwa moyo wao wa kukichangia kituo hicho, pia aliishukuru Serikali ya Awamu ya Tano kwa kufanya mambo mengi yanayoonekana.

“Tunafuraha sana kwa ujio wenu, tunashukuru sana kwa misaada mbalimbali mlioitoa, na pia tunaishukuru Serikali ya awamu ya tano kwa kufanya mambo mengi yanayoonekana, sisi tunasaidia serikali hii kwa sala zetu, hatupo katika siasa,”

IMEANDALIWA NA JOEL MADUKA. 
Share it:

habari

Post A Comment: