SERIKALI imewasilisha mbele ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya
Huduma za Jamii Muswada wa Huduma za Habari ikieleza kuwa ni sheria itakayoleta
mageuzi makubwa nchini.
Hayo yamesemwa na Waziri wa Habari Utamaduni Sanaa na Michezo
Mhe. Nape Moses Nnauye alipokuwa akiwasilisha muswada wa sheria hiyo leo mjini
Dodoma ambapo amesema sasa sekta ya habari inakwenda kuwa taaluma kamili.
Waziri Nnauye amesema Sheria hii italeta mifumo ya kisasa ya
usimamizi wa sekta ya habari na mifumo ambayo inaweza kugusa au kubadili namna
wanahabari walivyozoea kutenda au kufikirika kwa sasa lakini akasema sekta hiyo
iwe tayari kwa mabadiliko.
“Niwaombe wanatasnia wenzangu tuwe tayari kwa mabadiliko haya
ili taaluma yetu iheshimike na sisi wenyewe tuheshimike zaidi” alisisitiza Mhe.
Nnauye.
Aidha Mhe. Nnauye ametoa wito kwa wadau wote kuunga mkono
muswada huo utakaojadiliwa katika Bunge lijalo la Novemba mwaka huu.
“Tuko hapa kuboresha na sio kusuguana tukae tuiandae tasnia bora
zaidi kwa kupitia na kutoa maoni juu ya Muswaada huu wa Sheria ya Huduma za
Habari 2016” alifafanua Mhe. Nnauye.
Ameongeza kuwa kwa sasa hadi wakati wa Bunge lijalo Serikali ipo
tayari kupokea na kuyafanyia kazi maboresho yatakayolenga kufikia maono ya
muswada huu kutoka kwa wadau ili kuipa heshima stahiki sekta ya habari.
Alisema kuwa muswada huo licha ya huu utatatua changamoto za
kutotambulika kwa sekta ya habari kama taaluma kamili inayopaswa kuheshimiwa,
pia utatatua changamoto ya kukosekana vyombo madhubuti na huru vya usimamizi wa
tasnia.
Alisema kutokana na hayo muswada unapendekeza kuundwa kwa Bodi
ya Ithibati itakayoainisha sifa za mwanahabari na kuwasajili.
Aliitaja taasisi nyingine inayoundwa kuwa ni Baraza Huru la
Wanahabari ambalo litakuwa na wajibu wa kuandaa na kusimamia maadili ya
wanahabari na watawajibishana wenyewe kwa wenyewe.
Wasomi wanena
Mhadhiri wa Sayansi ya Siasa katika Chuo Kikuu cha Dar es
Salaam, Dkt. Benson Bana anasema kuwa kuja kwa sheria hiyo ni jambo la busara
kwa sababu kwa sasa weledi wa uandishi wa habari uko chini.
“Sheria hii iwe na makali zaidi kwa wanahabari ambao watakiuka
utaratibu na maadili. Hakuna nchi ambako wanahabari wanajiendea tu bila
uratibu,” alisema,
Alisema ni vyema na ni wakati mauafaka kwa sekta ya habari kuwa
taaluma kamili na kushauri kuwa wanaoitumikia fani hiyo kwa sasa wawe tayari
kwa mabadiliko.
Naye Mhadhiri wa Sayansi ya Siasa na Uhusiano wa Kimataifa wa
Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dkt William John Walwa alisema sheria imekuja
wakati muafaka na inapaswa kutatua changamoto za fani hiyo.
Post A Comment: