Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John
Pombe Magufuli ameagiza viongozi wote wa Serikali walioalikwa kuhudhuria
sherehe za Kilele cha Mbio za Mwenge wa Uhuru kitaifa zitakazofanyika tarehe 14
Oktoba, 2016 katika Wilaya ya Bariadi Mkoani Simiyu kutohudhuria sherehe hizo
na wale ambao walishalipwa fedha ya posho na safari kwa ajili hiyo wazirejeshe.
Taarifa iliyotolewa leo tarehe 12 Oktoba, 2016 Ikulu
Jijini Dar es Salaam na Katibu Mkuu Kiongozi Balozi John Kijazi imeeleza kuwa
Rais Magufuli ametoa maagizo hayo ikiwa ni utekelezaji wa azma ya Serikali ya
awamu ya tano ya kubana matumizi yasiyo ya lazima na kuelekeza rasilimali
nyingi katika shughuli za maendeleo ya nchi.
Viongozi waliotajwa kutakiwa kufuta safari zao za
kwenda Bariadi ni pamoja na Wakuu wote wa Mikoa, Wakuu wote wa Wilaya,
Wakurugenzi wote wa Mamlaka za Serikali za Mitaa, Mameya na Wenyeviti wote wa
Halmashauri za Majiji, Manispaa, Miji na Wilaya pamoja na watumishi ambao
huambatana nao wakiwemo madereva na wasaidizi wao ambao kwa idadi hufikia
takribani 1,500.
Kwa kuwa sherehe za Kilele cha Mbio za Mwenge wa Uhuru
huambatana na Maadhimisho ya Siku ya Kumbukumbu ya Muasisi wa Taifa na Baba wa
Taifa Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere aliyefariki dunia miaka 17
iliyopita, agizo hilo limewataka Viongozi wote wa Mikoa na Wilaya kubaki katika
maeneo yao ya kazi na kujiwekea utaratibu wa jinsi ya kuienzi siku hiyo.
Aidha, Rais Magufuli ameagiza Wilaya zote ambazo
zimefanya vizuri katika shughuli za maendeleo wakati Mwenge ulipokuwa katika
maeneo yao, zitambuliwe kwa kutangazwa rasmi katika siku ya kilele cha Mbio za
Mwenge na kwamba zawadi zilizoandaliwa zitapelekwa kwa wahusika kwa utaratibu
utakaoelekezwa na Mamlaka inayohusika kutoa zawadi hizo.
Hata hivyo Dkt. Magufuli ameelekeza kuwa kutokana na
umuhimu wa Mwenge wa Uhuru kwa Taifa, Viongozi wote wa Serikali ya Mkoa wa
Simiyu na Wilaya zake pamoja na wananchi wote wa mkoa huo wajitokeze kwa wingi
na kushiriki katika sherehe za kuzima Mwenge wa Uhuru siku hiyo ya tarehe 14
Oktoba, 2016.
Mgeni Rasmi katika sherehe za kuzima Mwenge wa Uhuru
atakuwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dkt. Ali
Mohamed Shein.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
12 Oktoba, 2016
Post A Comment: