Katibu
Mtendaji wa Bodi ya Filamu Tanzania Joyce Fissoo amesema serikali iko mbioni
kukamilisha sera ya maendeleo ya filamu ambayo inategemewa kuwa mwarobaini wa
changamoto zinazoikabili sekta hiyo yenye kutoa ajira kwa vijana wengi nchini.
Kauli ya
kiongozi huyo wa taasisi ya Serikali yenye dhamana ya kusimamia maendeleo ya
sekta ya filamu nchini aliitoa wakati akijibu swali la mtangazaji wa kipindi
cha Tunatekeleza, Esha Muhiddin, kinachorushwa na runinga ya TBC1.
Kwenye
mahojiano hayo mtangazaji alitaka kujua kama sheria Na. 4 ya Filamu na Michezo
ya Kuigiza ya mwaka 1976 inakidhi mahitaji ya sasa ambapo Bi. Fissoo alikiri
kuwa sheria hiyo ina upungufu kwenye baadhi ya maeneo ambayo ni ya muhimu kwa
ustawi wa tasnia ya filamu na uchumi wa nchi kwa ujumla.
Bi. Fissoo
alieleza moja ya upungufu wa sheria hiyo ni kushindwa kuwalazimisha
watayarishaji wa filamu kutoka nje ya nchi kutoa mgao wa faida wanazozipata
baada ya kutumia mandhari za Tanzania kwenye filamu zao. Upungufu huo
umesababisha nchi kukosa mapato ambayo yangeweza kutumika kwenye miradi
mbalimbali ya maendeleo.
Upungufu
mwingine wa sheria hiyo ya mwaka 1976 ni kuiona sekta ya filamu kama chanzo cha
burudani ambacho hakina thamani kwenye soko la bidhaa na huduma. Mtazamo huu
umepelekea wasanii wa filamu kushindwa kupata kipato wanachostahili.
“Baada ya
kutambua mapungufu hayo Serikali ya awamu ya tano imedhamiria kukamilisha sera
ya maendeleo ya filamu nchini ambayo itazaa sheria na kanuni zitakazokuwa tiba
ya changamoto zinazoikabili sekta ya filamu” Bi Fissoo aliongeza.
Mbali na
ujio wa sera ya maendeleo ya filamu nchini Bi. Fissoo aligusia maeneo mengine
ambayo serikali ya awamu ya tano kupitia Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na
Michezo na Bodi ya Filamu Tanzania yamefanikiwa kuyapatia ufumbuzi ikiwa ni
pamoja na kutoa mafunzo kwa wadau zaidi ya elfu moja kwenye mikoa mbalimbali
nchini.
Maeneo
mengine ni kuiboresha Bodi ya Filamu Tanzania tokea mwezi Julai 2016. Kwa sasa
Bodi ina mamlaka kamili na muundo mpya unaowezesha kusimamia majukumu mapya
yaliyoongezwa ili kuhakikisha sekta ya filamu inakuwa na mchango wa kutosha
kwenye ukuaji wa uchumi.
Katibu
Mtendaji huyo wa Bodi ya Filamu pia alitoa msimamo wa serikali kuhusu tabia ya
watayarishaji wa filamu za kizawa kuzigawa filamu zao kwenye sehemu mbili (part
1&2) kuwa ni kitendo kischokuwa na nia njema na kina lengo la kuhadaa
walaji wa filamu za kitanzania. Alibainisha tabia hiyo kuwa moja ya sababu za
kushusha soko la filamu za kitanzania ndani na je ya nchi.
Bi Fissoo
amewaasa wadau wa sekta ya filamu nchini kujitokeza kwa wingi kutoa mawazo yao ili
kuboresha sera ya maendeleo ya filamu nchini pale watakapo hitajika.
IMEANDALIWA NA ABUU KIMARIO
Post A Comment: