TAASISI YA VICTORIA YAZINDULIWA NA KUTOA MAFUNZO KWA WAJANE

Share it:

Picha mbalimbali zikionesha matukio wakati wa uzinduzi wa Taasisi ya Victoria Foundation uliofanyika hivi karibuni katika mji wa Geita ulioenda sabambamba na utoaji vyeti kwa washiriki wa mafunzo ya ujasiriamali.

Mafunzo ya ujasiriamali 
yametolewa kwa wanawake wajane na wasiojiweza wa mkoa wa Geita kupitia mfuko wa 
Victoria Foundation unaomilikiwa na mbunge wa viti maalum CCM, Vicky Kamata.
 
Mafunzo hayo yalitolewa kwa 
lengo la kupunguza pengo la elimu ya masuala ya fedha kwa wanawake hao kwa 
kuwafundisha mbinu mbali mbali za biashara, namna ya kuweka akiba na kulipa 
mikipo.
 
Akizungumza wakati wa uzinduzi 
wa mafunzo hayo, Mkuu wa mkoa wa Geita, Meja Jenerali Mstaafu Ezekiel Kyunga alimpongeza 
Kamata kwa jitihada zake kwa kuinua wanawake hususani wajane na wasiojiweza 
kiuchumi na kuwataka wanawake kujenga utamaduni wa kufuatilia taarifa mbali mbali kuhusiana na 
masuala ya fursa za kibiashara ili kuzitumia katika kupanua wigo wa shughuli 
zao.
 
Alisema wanawake wengi nchini wanashindwa kusonga mbele 
kibiashara kwa kuwa wanakosa taarifa ambazo zingetumiwa kuwawezesha kusonga 
mbele na kujikwamua kiuchumi.
 
“Ni wakati sasa kwa 
wanawake nchini kutafuta taarifa zitakazoinua biashara, mafunzo kama haya 
mmeyapata bure myatumie vema kuhakikisha mnatimiza malengo yenu.”alisema.
 
Kwa upande wa muandaaji wa 
mafunzo hayo, Vicky Kamata alisema mfuko wake mbali na kutoa misaada mbali 
mbali kwa walemavu, ni wakati sasa wa kusaidia elimu kwa wanawake na
kuwawezesha mitaji ili waweze kufikia lengo.
 
“Naamini mwanamke ni jeshi 
kubwa, ukimuwezesha mwanamke mmoja umewezesha jeshi kubwa lililopo nyuma yake  
hata watoto watasoma vizuri.”alisema Kamata
 
Awali  kupitia mfuko huo wa Victoria Foundation, 
awamu wa kwanza ya utekelezaji wa ahadi zake kwa wakazi wa Geita waliomsaidia 
kuchaguliwa kwake kuwa mbunge kupitia CCM , Kamata alitoa misaada ya  vyakula, mavazi, magodoro na viti vya 
walemavu (Wheel Chair) 30 kwa wakazi wa tarafa ya Bugando.
 
Alisema kupitia mfuko wa 
Victoria Foundation  wakazi wa Geita 
watanufaika kwa misaada mbali mbali itakayowawezesha watu hususani wanawake 
wajane na yatima na wale wasiojiweza kuondokana na adha walizonazo na kufurahia 
maisha kama watu wengine.
Share it:

habari

Post A Comment: