RAIS MAGUFULI ATOA ONYO KWA WAKUU WA MIKOA NA WILAYA NA WAKURUGENZI WA HALMASHAURI AWATAKA WAWE NA NIDHAMU YA PESA

Share it:
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akiwaonya wakuu wa wilaya na wakuu wa mikoa pamoja na wakurugenzi wa Halmashauri za Wilaya   nchini  kote kuachana na tabia ya kutumia fedha za serikali isivyotakiwa wakati wa  Mkutano ambao umefanyika kwenye  viwanja vya shule ya sekondari  Wilayani Chato 

Rais Mstaafu wa awamu ya tatu Mheshimiwa Benjamini Mkapa  ambaye ndiye alikuwa Mgeni Rasmi kwenye makabidhiano ya Nyumba za watumishi wa sekta ya afya akizungumza na wananchi ambapo amesisitiza watumishi waliopo kufanya kazi kwa kujituma zaidi.

Rais Mstaafu wa awamu ya tatu Mheshimiwa Benjamini Mkapa akimkabidhi hati za nyumba hamsini , Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Ummy Mwalimu

Rais Mstaafu wa awamu ya tatu Mheshimiwa Benjamini Mkapa akimkabidhi,mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Bukombe Nicas Safari hati ya nyumba za watumishi wa afya.

Mama Janeth Magufuli Akisalimiana na Balozi wa Japan hapa nchini Masaharu Yoshida mara baada ya kuwasili kwenye viwanja vya Mkutano Wilayani Chato.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akisalimiana na Mkuu wa Mkoa wa Geita Meja Jenerali Mstaafu Ezekiel Kyunga wakati alipowasili kwenye viwanja vya Mkutano.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akisalimiana na wananchi wa Wilaya ya Chato.

Mtendaji Mkuu wa  Mkuu wa taasisi ya Benjamini Mkapa Ellen Senkoro ,akielezea makusudi ya kujenga Nyumba hizo kwenye Mikoa ya Kagera,Simiyu na Geita.

Mbunge wa Chato ambaye pia ni Naibu Waziri wa Nishati Mheshimiwa Medadi Kalemani akizungumza na wananchi na kushukuru serikali kwa kuendelea kuwekeza kwenye Sekta ya afya.

Madiwani wa kata mbali mbali Mkoani Geita.

Wake Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Ummy Mwalimu akielezea mikakati ya kuendelea kuboresha sekta ya afya.


Wananchi wa wilaya ya Chato na Wilaya zilizopo Mkoani Geita wakifuatilia Mkutano wa Kiongozi wa Nchi.                 

 Picha na Joel Maduka


Rais Magufuli amesema hayo leo wilayani  Chato mkoani Geita alipokuwa akihutubia wananchi katika makabidhiano ya nyumba 50 zilizojengwa na taasisi ya Benjamin Mkapa, ambapo mbali ya kushukuru kwa msaada huo Rais Magufuli alizungumzia juu ya tabia ya baadhi ya viongozi wa serikali kuiba fedha za wananchi na kutumia katika mambo yao wenyewe nje ya malengo ya serikali.

"Hapa penyewe Chato kuna fedha zaidi ya bilioni moja za pembejeo zimeliwa na viongozi, hivyo natoa wito kwa viongozi wote wakuu wa wilaya na wakuu wa mikoa kote nchini kuwa na nidhamu na fedha za serikali, tujifunze kutumia fedha vizuri  za serikali asitokee mchwa huko kula pesa za serikali. Maana hili lililotokea hapa Chato najua limetokea sehemu nyingi na hivyo saizi tunaanza kufanya ukaguzi kila sehemu"alisema Rais Magufuli.

Mbali na hilo Rais Magufuli aliwataka wananchi wa hali ya chini kuwa na amani kwani katika kipindi chote ambacho yeye atakuwa madarakani hataki kuona wala kusikia wananchi wa hali ya chini wakinyanyaswa sababu na yeye ametokea katika maisha hayo hivyo anatambua jinsi wanavyopata shida watu wa kipato cha chini.

"Serikali haiwezi kufanya biashara na masikini, inawaacha matajiri inawasumbua masikini, mimi nimekuwa katika maisha ya shida nimechunga ng'ombe, nimeuza maziwa kwa hiyo najua maisha ni nini. Najua Tanzania watu wengi wanaishi maisha ya chini na katika kipindi changu sitaki kuona watu wa hali ya chini wanapata shida, wanapata taabu ndiyo maana tunajitahidi kuhangaika kuleta maendeleo ili wanufaike na wao" alisisitiza Magufuli

Rais Magufuli akuziacha taasisi ambazo zimekuwa zikitetea wanafunzi kupata mimba na kusema yeye taasisi hizo hazipendi na ameziwekea kizingiti kuwa ikiwezekana zisipewe msaada bali taasisi zinazofanya mambo ya kimaendeleo kama taasisi ya Mkapa Foundation ndiyo zinatakiwa kupewa msaada sana kwa kuwa zinarudi kuleta maendeleo kwa wananchi.


Aidha Kwa Upande Wake Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Ummy Mwalimu amesema Wizara ya Afya inatarajia kuanza kutoa huduma ya kupandikiza figo katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili na kuwapunguzia changamoto wagonjwa kusafiri umbali mrefu nje ya Nchi na matumizi ya pesa nyingi kugharamia matibabu
Aidha kwa Upande wake Rais Mstaafu  wa awamu ya Tatu ambaye ndiye alikuwa Mgeni Rasmi kwenye Makabidhiano hayo Benjamini Mkapa,amesema kuwa anatambua kuwa bado nchi inauhaba wa wahudumu wa afya lakini amewataka wale ambao wapo kwa sasa ni vyema kuakikisha wanajituma na kufanya kazi kwa uhadilifu Mkubwa na kwa waledi katika kutoa huduma  kwa wananchi .

Mtendaji Mkuu wa  Mkuu wa taasisi ya Benjamini Mkapa Ellen Senkoro amefafanua kuwa  nyumba hizo ambazo zimejengwa kwenye Mikoa ya Simiyu ,Geita na Kagera ni juhudi ya taasisi hiyo kwa kushirikiana na serikali kupunguza vifo vya wakina mama na watoto hasa ambao wanaishi maeneo ya vijijini.



IMEANDALIWA NA MADUKA ONLINE

Share it:

habari

Post A Comment: