WANANCHI MEATU WAHAMASIKA KUCHANGIA ELIMU KUBORESHA MIUNDOMBINU.

Share it:
John pang'wa, Afisa Elimu msingi wilani Meatu mkoani Simiyu akiongea na waandishi wa habari hawapo pichani juu ya utatuzi wa changamoto za elimu hasa ujenzi wa madarasa, vyoo na nyumba za walimu.
Jengo la nyumba ya mwalimu shule ya msingi Mwamalole liliojengwa kwa nguvu za wananchi lenye uwezo wa kukaliwa na familia mbili za walimu endapo litakamilika.

Wanafunzi wa shule ya Msingi Mwamalole wakiwa shuleni.

Majengo ya shule ya Msingi Nyanza, shule hiyo inakabiliwa na uhaba wa madarasa, hali inayofanya wanafunzi kusoma nje na chini ya mti wa Mbuyu.


Wajumbe wa UWW shule ya msingi Nyanza, wakiwa katika kikao cha kujadili maendeleo ya shule.


Wanafunzi wa shule ya Msingi Mwamamole wilayani Meatu mkoani simiyu, wakiwa wanasoma darasani.

Mwenyekiti wa kijiji cha Nyanza, Mbuke Masalu akiongea na wajumbe wa UWW katika kikao cha kujadilia maendeleo ya shule ya msingi nyanza juu ya ujenzi  wa madarasa, vyoo na nyumba za walimu.  (PICHA ZOTE NA COSTANTINE MATHIAS).


NA COSTANTINE MATHIAS, MEATU.

Uhaba wa Miundombinu ya Elimu ya madarasa, vyoo, nyumba za walimu ni moja ya vikwazo katika sekta ya elimu wilayani Meatu mkoani Simiyu, hali inayofanya ufanisi wa sekta hiyo kuwa duni.

Wajumbe wa Ushirikiano wa Walimu na Wazazi (UWW) wilayani humo, wanasema kuwa kupitia ushirikiano huo  wameanza kuhamasisha jamii kuboresha miundombinu ya madarasa na nyumba za walimu kwa kutambua kuwa shule ni mali ya jamii.

Daud Mabeja mwenyekiti wa UWW kijiji cha Nyanza alisema kuwa wanafunzi wa shule hiyo walikuwa wakisomea  chini ya mbuyu kwa muda mrefu kutokana na uhaba wa madarasa, kwa sasa wamechangia na kufanikiwa kujenga madarasa.

‘’tulihamasishana kuunganisha nguvu kati ya wananchi na shule, tulileta mawe, maji na mchanga…kamati ya shule ilichangia fedha tukaanza ujenzi wa madarasa mawili na ofisi moja’’ alisema Monika Mwinula.

Mwenyekiti wa kijiji cha Nyanza Mbuke Masalu alisema kuwa wananchi siyo wagumu kuchangia endapo viongozi wakiwa wakweli…kutokana na fedha ya pamba ya shule na michango ya wananchi tumefanikiwa kujenga hayo madarasa.

Mwalimu mkuu wa shule ya msingi Mwamalole Joseph Machemu alisema kuwa tangu shule hiyo ianzishwe walimu wamekuwa wakiishi mbali na shuleni, hali inayowafanya kushindwa kufanya kazi kwa ufanisi, kwa ukosefu wa nyumba za walimu.

‘’mmoja wa walimu alikuwa akiishi nyumba ya kupanga, bahati mbaya akaingiliwa na nyuki uvunguni mwa kitanda na nyuki hao walikuwa ni zindiko la mwenye nyumba, mwalimu alishindwa kuwafukuza...baada ya siku tatu mwenye nyumba alikuja kuwatoa, kwa hiyo walimu wanakumbana na changamoto nyingi sana’’.

Ndilanha loya mjumbe wa UWW Mwamalole alisema kuwa tangu mwaka 1972 shule hiyo haijawahi kuwa na nyumba ya mwalimu hata moja, lakini kutokana na kuunganisha  jamii wameweza kujenga nyumba ya mwalimuyenye uwezo wa kukaliwa na familia mbili.

‘’kila kaya ilichangia silingi 31,250/=, kujitolea nguvu kazi, kusomba mawe, kufyatua tofali…hali hiyo ilitufanya tuweze kujenga nyumba ya mwalimu hadi usawa wa lenta na tunaiomba serikali itusaidie kuimalizia’’ alisema Loya.

Kwa upande wake Afisa Elimu msingi John Mpang’wa alisema kuwa mingoni mwa wilaya zenye mazingira magumi ni meatu, hivyo jukumu la kuchangia elimu ni la wananchi na kuongeza kuwa mahitaji ya miundombinu ni makubwa kuliko uhalisia uliopo.

Alisema kuwa  wana shule za msingi 111 za serikali na moja ya binafsi, wanahitaji vyumba vya madarasa 1639 na yaliyopo ni 884  huku wakiwa na upungufu wa vyumba 755 hali inayowafanya wanafunzi wengi kusomea chini ya miti.

Aliongeza kuwa wanahitaji nyumba za 1639, zilizopo ni 339 na upungufu wa nyumba 1300 hali inayowafanya walimu wengi kushindwa kuyamudu mazingira kutokana na jiografia kuwa si rafiki.

‘’tunashirikiana na jamii kwa kuhamasisha kuchangia ukarabati na ujenzi wa miundombinu kupitia Ushirikiano wa Wazazi na Walimu (UWW), ili tuweze kuboresha mazingira ya kujifunzia na kufundishia’’ alisema Mpang’wa.

Wilaya ya Meatu ina jumla ya wanafunzi wa shule za msingi 64,894, wavulana wakiwa ni 31,597 na wasichana 33,300, na ina walimu 1,166, wana wake wakiwa 434 na wanaume 732 huku mahitaji yakiwa ni walimu 1,844 na kufanya upungufu wa walimu 678.


Share it:

habari

Post A Comment: