NA JOEL MADUKA.
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na
Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa, amewataka wananchi wa mkoa wa Geita
kutumia fursa ya ujenzi wa Uwanja wa ndege wa kisasa wa Geita
kujikomboa kiuchumi.
Profesa Mbarawa aliyasema hayo mapema leo
wakati alipokuwa akiweka jiwe la msingi la uwanja huo katika kijiji cha Nyabilezi
mkoani Geita na kusisistiza kila mwananchi kuangalia namna
atakavyonufaika na uwanja huo.
“Serikali imejipanga kuhakikisha
kwamba usafiri wa anga unaimarika ili kurahisisha huduma ya usafirishaji
wa abiria, hivyo kuvutia watalii katika vivutio mbalimbali nchini”,
amesema Profesa Mbarawa.
Aidha, Profesa Mbarawa, amewataka
wakazi wa Kanda ya Ziwa, kutumia fursa ya uwepo wa Uwanja wa ndege huo
kukuza utalii, kilimo, ufugaji na biashara ya madini ili kuhuisha uchumi
wa mikoa ya Kanda ya Ziwa.
Waziri Mbarawa aliongeza kuwa
katika kuhakikisha Usafiri wa anga nchini unaimarika Serikali
imekarabati Viwanja vya ndege vya Mpanda, Bukoba, Tabora na Mafia na
ina mpango wa kuvijenga kwa kiwango cha kisasa viwanja 11 nchini ili
kuwezesha ndege mpya za Shirika la Ndege (ATCL), kutoa huduma katika
mikoa mbalimbali.
Kwa upande wake, Mtendaji Mkuu wa
Wakala wa Barabara nchini (TANROADS), Mhandisi Patrick Mfugale, alisema
ujenzi wa Uwanja wa Ndege wa mkoa wa Geita ni sehemu ya utekelezaji wa
sera ya usafiri wa anga nchini ya mwaka 2003 inayooelekeza uwepo wa
uwanja wa ndege wa kisasa katika kila mkoa ili kurahisisha uchukuzi na
kuchochea fursa za kibiashara na kitalii katika maeneo mbalimabali ya
nchi.
Mhandisi Mfugale, aliongeza kuwa
Uwanja wa Ndege wa Geita ambao unajengwa na Kampuni ya kikandarasi ya
Mayanga ambayo ni ya mzawa kwa gharama ya zaidi ya Shilingi Bilioni 41.
“Uwanja huu utakapokamilika
utawezesha ndege kubwa aina ya Boeing 737 – 800 zenye uwezo wa kubeba
abiria 100 hadi 200 kuruka na kutua, hivyo kuongeza na kurahisisha
huduma ya usafiri wa anga katika Ukanda huo”, amesema Mhandisi Mfugale.
Naye, Mkuu wa Mkoa wa Geita,
Mhandisi Robert Luhumbi, alisema wamejipanga kutumia uwanja wa ndege wa
Geita katika kukuza utalii na biashara mkoani humo na kuahidi kuulinda
uwanja huo na kutunza miundombinu yake.
Uwanja wa Ndege wa Geita wenye
urefu wa Kilometa 3 na upana wa Meta 45 unatazamiwa kuwa na uwezo wa
kuegesha ndege kubwa Tatu kwa wakati mmoja pindi utakapokamilika.
Post A Comment: