SOMO MUHIMU KWAKO

Share it:




SOMO MUHIMU KWAKO
Kwa muda mrefu watu wamekuwa wakiniuliza kwa nini nimefanikiwa, kwa nini nimetoka katika hatua fulani na kuingia katika hatua fulani. Nimekuwa nikiwajibu kwamba kujituma kwangu ndiyo kumenifanya kuwa hapa, kutokulala kwangu kwa muda mrefu huku nikifikiria ni kitu gani natakiwa kufanya ili nitoke kutoka hapa nilipo.
Katika kuwaambia hayo lakini pia huwa siwafichi kuhusu siri moja muhimu ambayo ilinifanya nitoke kule kwa haraka na kuja huku. Kitu hiki ndicho nitakachokwambia leo, nitataka ufanikiwe, sitaki ubaki hapo ulipo, mbegu nitakayoipanda moyoni mwako leo, nitataka ikue moyoni mwako na kuota mizizi.
Kuna kipindi sikuwa nikipenda mitandao ya kijamii kwa sababu nilijiona kuwa bize sana. Baada ya kipindi fulani, nikapata wazo la kuwaambia vijana kuhusu maisha yangu, wale waliokata tamaa, basi niwatie nguvu na kuendelea mbele.
Najua si wote wanaosoma magazeti, si kila siku nitapata nafasi kwenye gazeti. Wakati mwingine nakuwa na kitu, nikiwaambia wafanyakazi wangu ambao ni kama ndugu zangu, wananiambia kwamba nafasi imekuwa ngumu kupatikana gazetini, hivyo natulia na kufikiria siku nyingine.
Wazo la kujiunga na mitandao ya kijamii likanijia. Kama yule Michael aliyekuwa kule kusipofika magazeti, lakini si ana simu? Si anatumia Facebook? Kwa nini nisizungumze naye? Labda Esta ni mgonjwa, hawezi kutoka ndani na kwenda kununua gazeti, lakini si ana simu? Si anatumia Facebook? Kwa nini nisizungumze nao na kupitia hukohuko Facebook? Kweli nikafungua hii page.
Ndugu yangu! Nimefungua page hii kwa ajili yako, sikufungua kwa ajili ya Obama, sikufungua kwa ajili ya Bill Gates, nimefungua kwa ajili yako, Mtanzania ambaye unatamani kutoka hapo ulipo, nimefungua page hii kwa sababu nina mambo mengi ya kuzungumza pamoja nawe, kukushauri ni kipi unachotakiwa kufanya.
Rafiki yangu! Hakuna siri kubwa katika utajiri kama UTOAJI. Wazazi wangu walinifundisha kuhusu kutoa, waliniambia kwamba hata kama sitokuwa na kiasi kikubwa cha fedha, ni lazima nitoe kwa wale ambao hawana kitu.
Hilo limekuwa somo bora katika maisha yangu. Nimekuwa nikifanya hivyo mara kwa mara, nimefundishwa kutoa na hivyo huwa ninawafundisha watu kuhusu utoaji.
Mungu anapotaka kumsaidia mama Halima ambaye ni masikini wa kutupwa, hamuangushii fuko la pesa mwanamke huyo mjane, anachokifanya ni kumsaidia mama Halima kupitia wewe. Mungu anampa mama Halima kupitia wewe hapo, je, utakapopewa fedha za mama Halima, utazila au utakwenda kumpa?
Wengine wanahisi kwamba kutoa ni lazima uwe tajiri, wengine wanajiona hawawezi kutoa, wanamuona Mengi, Bakhresa ndiyo watu wanaotakiwa kutoa na si wao. Ndugu yangu, hakuna baraka nyingi kama kwenye utoaji. Ni bora kutoa kuliko kupokea.
Unapotoa, Mungu hakuachi hivihivi, atakubariki maradufu. Wakati mwingine unaanzisha biashara, haziendi, kila unapoanzisha, zinafeli, umekuwa ukijiuliza tatizo ni nini, unahisi umerogwa kisa tu kuna siku ulikuta unyoya wa kuku mlangoni kwako, unahisi kuna mtu hataki ufanikiwe, kumbe ukifuatilia ni kwa sababu wewe si mtoaji.
Mungu ametamani kuwasaidia watu wengi kupitia wewe, anakupa lakini hupeleki kunapotakiwa kwenda, mwisho wa siku, unatumia fedha zote na hapo bado unataka Mungu akufanikishe katika biashara zako.
Ndugu yangu, Mungu hafanyi kazi kwa staili hiyo. Mungu anataka akupe wewe, na wewe utoe kwa watu wengine. Kuna somo pana kuhusu utoaji na limekuwa likiwasaidia watu wengi.
Waangalie matajiri wengi, nampongeza Reginald Mengi, amekuwa mtu wa kujitoa, anasaidia wengi, kila mwaka huwa anawaita walemavu na kula nao. Ni jambo jema na huwa Mungu analiangalia sana jambo lake, na hata baraka anazozipata ni kwamba huwa anatoa.
Nimekuwa kwenye msingi wa kutoa, najua fedha anazonipa Mungu si zangu zote, nyingine huwa ni za mama Petro ambaye amekuwa akipigwa na umasikini mkubwa, nyingine huwa ni za yule mjane anayesoma na kushindwa kulipia ada.
Mungu yupo tayari kukufanya kuwa bilionea, lakini kabla hajakupa bilioni tano, je, alipokupa elfu kumi ulifanya jambo gani kwa ajili ya wengine? Wengine wanakuwa na nguo nyingi, zinapochakaa au kutokuwatosha, wanazitupa.
Ndugu zangu! Hakuna nguo chakavu duniani. Ile ambayo wewe unaiona chakavu, kuna watu kwao ni nguo mpya kabisa. Wagawie na watakutakia baraka katika maisha yako.
Wengine mnakula chakula mpaka mnabakiza na kukimwaga. Unajua wangapia hawajala? Unajua wangapi wana siku mbili hakuna kitu kilichoingia tumboni mwao?
Unasema upo bize, lakini kila wikiendi unakwenda kuangalia filamu Mlimani City au Dar Free Market, hivi umekwishawahi kwenda hata katika kituo cha watoto yatima ukawajulie hali?
Wakati mwingine si kuwapa fedha, kwenda kuwajulia hali, inatosha. Umekwishawahi kufanya hivyo? Mwisho wa siku unasema hakuna ajira, lakini cha kushangaza, baadhi ya marafiki zako wanaajiriwa.
Ndugu yangu, uasipotoa kwa ajili ya wenye uhitaji, naye Mungu anakufichia ajira. Kuna sehemu kuna kazi, unakuwa wa kwanza kupeleka barua lakini anachukuliwa mtu wa mwisho, tena hana sifa nzuri kama zako. Unajua kwa nini? Mungu yupo kazini, anamchukua mtu anayejali wengine na kukuacha wewe.
Umepeleka barua zaidi ya sitini kwenye makampuni tofautitofauti, cha ajabu huitwi kufanya kazi lakini wengine wanaitwa. Badilika, anza kumtolea Mungu kwa kuwasaidia wengine.
Kuna siri kubwa sana kwenye utoaji. Matajiri wanaongezewa zaidi kwa sababu wao wanatoa, kwa sababu wao wanasaidia wengine. Wakifanikiwa, tunajisemea kwamba mwenye nacho huongezewa, tena tunajisema kwa kusema ng’ombe wa masikini hazai.
Ukitaka kuona mafanikio katika biashara yako, anza kutoa, wasaidie masikini hata kwa kuwanunulia sukari kilo moja halafu utaona ni kwa jinsi gani Mungu atakufunulia baraka kubwa katika maisha yako.
Kwa leo ni hilo tu. Kumbuka.....kuwasaidia wengine ndiyo mlango mkuu wa mafanikio.
Na E.J SHIGONGO
Share it:

Darasa huru

Post A Comment: