HALMASHAURI ZISIZOKAMILISHA MADAWATI KIKAANGONI

Share it:







WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), George Simbachawene ameiagiza mikoa yote ambayo bado inakabiliwa na uhaba wa madawati kuhakikisha ifikapo Januari mwakani iwe imekamilisha, vinginevyo watakuwa wameonesha kushindwa kuendana na kasi ya Serikali ya Awamu ya Tano.

Alitoa kauli hiyo jana jijini Dar es Salaam wakati akipokea msaada wa madawati 3,500 kwa shule za msingi na sekondari yaliyotolewa na benki ya NMB.

Aliitaja mikoa iliyokamilisha kampeni ya upatikanaji wa madawati ni Dar es Salaam, Mtwara, Lindi, Arusha, Iringa, Kilimanjaro, Mbeya, Manyara, Njombe, Pwani, Ruvuma, Shinyanga, Singida na Tabora. Aliongeza kuwa, mikoa ya Geita, Mwanza, Kigoma, Mara, Rukwa, Simiyu na Dodoma haijakamilisha.

“Ipo mikoa sijaitaja, hiyo imebakisha kiasi kidogo na najua wataweza kukamilisha kwa muda mfupi, lakini niseme hao ambao bado nataka wahakikishe wanakamilisha na Januari ni lazima kila mkoa uwe umekamilisha, tofauti na hapo tutawaona wameshindwa kabisa kwenda na kasi hii,” alieleza Simbachawene aliyeishukuru benki hiyo kwa kusaidia madawati.

Naye Mkurugenzi Mkuu wa NMB, Ineke Bussemaker alisema madawati hayo yatasambazwa katika shule za msingi na sekondari 71 nchini na kila shule itapata madawati 50.

Alisema katika miaka mitano, benki hiyo imesaidia madawati 15,000 yenye thamani ya Sh bilioni 1.5.
Share it:

habari

Post A Comment: