JESHI la Polisi Wilayani
Bukombe Mkoani Geita limemfikisha Mahakamani Abdulazizi Mohamed mkazi wa
Runzewe kwa kosa la unyang’anyi wa kutumia Silaha kisha kupora Pikipiki.
Mbele ya Hakimu Mkazi
Mfawidhi ,Mwandamizi wa Mahakama ya Wilaya ya Bukombe Gabriel Kulwijira
mwendesha mashitaka wa Polisi Lazaro Mhegele mahakamani hapo alisema mshitakiwa
Abdulazizi anashitakiwa kwa kosa la unyang’anyi wa kutumia silaha kinyume na
kifungu Na 287 A cha sheria ya kanuni ya adhabu sura ya 16 iliyofanyiwa
marejeo 2002 na kufanyiwa marejeo tena kwa sheria Na 3/2011.
Mhegele alisema mshitakiwa
abdulazizi alitenda kosa hilo septemba 11, 2016 majira ya saa 2.30 usiku katika
kijiji cha Busonzo akiwa na mwenzake waliiba Pikipiki yenye namba
za usajili MC 622 BKB yenye thamani ya Sh.1950,000 mali ya Omari Shaban
mkazi wa kijiji cha Runzewe.
Akizungumzia mazingira ya
Tukio hilo mwendesha mashitaka huyo wa polisi alisema mshitakiwa na
mwezake walikodi Bodaboda hiyo iliyokuwa ikiendeshwa na dereva Hamis Charles
(20) ili awapeleke kijiji cha Busonzo kwa mganga wa kienyeji majira ya saa 11
jioni akawapeleka na ilipofika saa 2.30 usiku walimpigia simu awafuate huko kwa
sangoma akawafuata na waliponza kurudi walipofika njiani wakamwambia asimame
akasimama kisha wakaanza kumshambulia kwa mapanga hadi akazirahi nao wakafikiri
kuwa ameshapoteza maisha wakachukua pikipiki hiyo na kutokomea kusikojulikana.
Alisema mungu si Athumani
dereva bodaboda huyo alizinduka na akapata fahamu akajikongoja kwa nguvu za
wasamaria wema hadi kituo cha Polisi Runzewe akaripoti kwani kati ya hao
waporaji alimtambua Abdulazizi Mohamed akawapeleka hadi anapofanyia kazi
zake mjini Runzewe na kisha uwamuzi wa
kukamatwa ndipo ulifanyika
Mnamo septemba 27, 2016
alifikishwa mahakama ya wilaya na kusomewa mashitaka yanayomkabili mshitakiwa
alikana shitaka ndipo Hakimu Gabriel Kulwijira aliiahirisha kesi hiyo hadi
oktoba 10 ,2016 itakapo tajwa tena.
Na Peter Makunga
Post A Comment: