MBEYA: Mwanafunzi
aliyeshambuliwa na walimu watano wa Shule ya Sekondari ya Kutwa ya Mbeya,
Sebastian Chinguku, aliwekwa ofisini kwa takribani saa tano baada ya kupata
kipigo hicho kilichoibua mjadala nchi nzima.
Tukio hilo liliibua mjadala
baada ya picha za video kusambaa kwenye mitandao ya kijamii katikati ya wiki na
kusababisha Serikali kuwatimua walimu hao waliokuwa wameenda shuleni hapo kwa
mafunzo ya vitendo.
Picha hizo zinawaonyesha
walimu hao wakimkamata mwanafunzi huyo mikono yote, baadaye kumpiga ngwala na
kuanza kumpiga kwa makofi, ngumi, mateke na fimbo, huku mmoja wao akionekana
kushughulika kumpiga kichwani mithili ya mtu anayeua nyoka.
Kumekuwa na maelezo tofauti
kuhusu tukio hilo, baadhi wakisema mwanafunzi huyo alionyesha kiburi alipotakiwa
apige magoti kama adhabu ya kutofanya zoezi la Kiingereza alilopewa na mwalimu
wake, Frank Msigwa.
Lakini habari ambazo
Mwananchi imezipata zinasema kuwa baada ya kufikishwa ofisini, mwanafunzi huyo
alionyesha utovu wa nidhamu uliosababisha walimu hao kufanya vitendo vya
kikatili vya kumchangia kumpiga na baadaye kumuweka ofisini kuanzia saa 3
asubuhi hadi saa 8 mchana wakati kengele ya kutoka ilipopigwa.
Walimu hao, ambao walikuwa
shuleni hapo kwa ajili ya mafunzo ya vitendo waliingia ofisini wakiwa wamemshika
mwanafunzi huyo na baadaye kumtaka apige magoti, lakini akakataa kufanya hivyo.
“Sikujua walikoanzia ila
niliona wazi hakukuwa na amani. Mwanafunzi aliambiwa piga magoti, akakataa,
wakambadilishia adhabu na kumwambia akae chini, lakini pia akagoma sisi bado
tukawa tumepigwa na bumbuwazi,” alisema shuhuda aliyezungumza na Mwananchi.
“Kitendo hicho
kilisababisha walimu hao kutumia bakora kumchapa, lakini yule Sebastian akawa
anashika fimbo na hapo ndipo walimu hao vijana walipoamua kushirikiana kwa pamoja
kutumia nguvu kumlaza chini na kumpiga.”
Baada ya Sebastian
kuadhibiwa kwa kipigo hicho kisicho cha kawaida shuleni, walimu hao walimchukua
kwa ajili ya kumrudisha darasani, lakini wakiwa njiani alitaka kukimbia.
“Kitendo hicho kiliwafanya
wamrudishe ofisini na kumuita mwalimu wa nidhamu ambaye alielezewa hali
ilivyokuwa, naye akamuita makamu mkuu wa shule ambaye alimtaka mwanafunzi
aandike barua ya kuomba msamaha,” alisema shuhuda huyo.
Alisema baada ya hapo
walimu hao walimtaka Sebastian akae ofisini hadi watakapomuhitaji. Mwanafunzi
huyo alilazimika kukaa ofisini hadi kengele ya kutoka ilipogongwa saa 8:00
mchana.
Uchunguzi wa Mwananchi
unaonyesha kuwa hiyo haikuwa mara ya kwanza kutokea tukio kama hilo.
“Ilishawahi kutokea
mwanafunzi alichelewa shule na kuamua kuruka ukuta, lakini walimu walimuona
wakamwita na kutaka kumuadhibu, akakataa huku akitaka kurusha ngumi. Ilibidi
walimu wengine wajongee eneo la tukio ili kumdhibiti,” alisena shuhuda huyo.
“Wakati huohuo simu
ikapigwa polisi ambao walikuja na gari wakamchukua kilichoendelea
sikufuatilia.”
Katika tukio la wiki hii,
Sebastian ametoa maelezo tofauti katika mazungumzo na Mwananchi jana. Amedai
kuwa baada ya tukio hilo, mwalimu mkuu msaidizi alimtaka aandike barua ya
kujieleza kwa madai ya utovu wa nidhamu aliouonyesha.
Alisema wakati anapigwa na
walimu hao wa chuo, walimu wengine walikuwa kwenye kikao ofisi ya taaluma
na baada ya kupigwa, walimgeuzia kibao wakidai kuwa yeye ndiye
aliyewashambulia.
“Waliwaeleza walimu
waliokuwa kwenye kikao kuwa mimi ndiyo nimewapiga na ndipo makamu mkuu wa
shule akaniamuru niandike barua ya kujieleza kwa utovu wa nidhamu,” alisema
Sebastian.
Alisema kabla ya kuanza
kuandika barua hiyo, alikuja mwalimu wa zamu na akamweleza hali halisi na
alimtaka aandike barua ya kuelezea tukio zima lilivyokuwa, wakati mwalimu
akipeleleza kwa wanafunzi wengine ili kujua ukweli.
“Baada ya kuandika
barua nikaitwa ofisi ya taaluma na wakanieleza kuwa wamebaini ukweli kuwa
walimu ndiyo walionipiga na ndipo walimu wengine wakaanza kunipa pole na
kunishauri nirudi nyumbani kutibiwa,” alisema.
Alisema tukio hilo
lilimfanya ahofie kuwa angefukuzwa shule baada ya kugeuziwa kibao, hadi akaona
awaambie kuwa amesamehe ili aweze kuendelea na shule.
“Ninachojua ukiambiwa
uandike barua ya kujieleza ni lazima ufukuzwe shule au usimamishwe na hilo
ndilo ilikuwa hofu yangu kubwa na ndiyo maana niliwaambia walimu kuwa
nimesamehe,” alisema.
Kuhusu suala la kushiriki
makundi ya wavuta bangi, mwanafunzi huyo alisema anashangazwa na tuhuma hizo
ambazo alishawahi kupewa hadi kutakiwa aandike maelezo na alipofanya hivyo,
shauri hilo likaisha.
Baba mzazi wa mwanafunzi
huyo, John Chinguku alisema amesikitishwa na ujumbe unaosambaa katika mitandao
ya simu kuwa Sebastian aliwahi kumjibu vibaya mbele ya walimu alipokuwa
amekwenda kumtetea asifukuzwe shule.
Pia tuhuma kuwa aliwahi
kuvunja televisheni na kwamba baba yake hamtaki nyumbani.
“Maelezo hayo si ya kweli
ni upotoshaji...kwangu sina hata umeme. Bado naendelea na ujenzi wa nyumba
yangu. Na huo ujumbe wa kuwa simtaki Sebastian si kweli kwa kuwa ni kijana
ninayemtegemea kwa kazi za nyumbani, hasa kusimamia ujenzi wa nyumba,” alisema.
Pia aliukana ujumbe
mwingine ambao alisema umesambaa mitandaoni kuwa anaomba msada wa matibabu na
kutaja namba ya simu na akaunti ya benki.
“Sihusiki na ujumbe huo
wala hakuna mahali popote nilipoomba msaada kwa kuwa mimi ni mtumishi wa benki
ya NMB. Kama masuala ya matibabu kwa mtoto wangu, yamefanywa na mwajiri wangu,”
alisema.
Kamanda wa
polisi mkoani hapa, Dhahiri Kidavashari alisema jeshi hilo linashikilia
watu wanane kwa mahojiano, wakiwamo walimu hao na kwamba uchunguzi unaendelea.
Post A Comment: