Waziri wa ujenzi, Uchukuzi na
Mawasiliano, Prof. Makame Mbarawa, akitoa maelekezo kwa uongozi wa Wilaya ya
Kibondo,alipotembelea ofisi hizo mkoani Kigoma.
|
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na
Mawasiliano Prof. Makame Mbarawa, akisikiliza taarifa kutoka kwa Mkuu wa Wilaya
ya Kasulu, Kanali Martin Mkisi mara baada ya kutembelea ofisi hizo mkoani
Kigoma.
|
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Prof.
Makame Mbarawa, akikagua moja ya vifaa vinavyotumika kupima aina ya udongo
unaotumika kujengea barabara katika maabara iliyopo kwenye kambi ya Mkandarasi
anayejenga barabara ya Kidahwe-Kasulu KM 50. Wa Pili Kulia ni Mhandisi wa
Maabara kutoka kampuni China Railway 15th Group Eng. Raphael Ndimbo.
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa
Makame Mbarawa ametoa agizo kwa Wakala wa Barabara nchini (TANROADS),
kushirikiana na Jeshi la Polisi pamoja na wananchi kuwabaini na kuwachukulia hatua kali za
kisheria madereva wote wa malori ya mchanga na kokoto watakaobainika kutofuata sheria za ubebaji wa
bidhaa hiyo na hivyo kusababisha uharibifu wa miundombinu ya barabara.
Waziri Mbarawa ametoa agizo hilo mkoani Kigoma
katika ziara yake ya kukagua barabara ya Kidahwe-Kasulu yenye urefu wa
kilometa 50 ambapo pamoja na mambo mengine amesema Serikali inatumia fedha nyingi
kujenga miundombinu ya barabara kwa maendeleo ya wananchi na Taifa kwa ujumla
hivyo haita mvumilia mtu yeyote atakayebainika kuharibu miundombu hiyo kwa
makusudi.
“Kuanzia sasa Serikali haitavumilia madereva
wasiozingatia kanuni na sheria za usafirishaji wa mizigo katika barabara
nchini, hivyo nawaagiza Mameneja wa TANROADS katika mikoa yote nchini kusimamia
sheria ili kudhibiti miundombinu ya barabara, amesema Prof. Mbarawa.
Aidha, Profesa Mbarawa ameliomba Jeshi la Polisi
kushirikiana vema na makandarasi wanaojenga miundombinu ya barabara katika
maeneo mbalimbali nchini kuwakamata na kuwachukulia hatua za kisheria baadhi ya
watu wasio waaminifu ambao wanaiba vifaa vya makandarasi jambo linalochangia
kukwamisha shughuli za ujenzi wa barabara.
Amewataka wananchi wa Wilaya ya Kasulu kutoa
ushirikiano kwa mkandarasi wa kampuni ya China Railway 15 Bureau Group
Corporation anayejenga barabara hiyo ili kuwezesha ujenzi huo kukamilika
haraka.
Naye Meneja wa TANROADS mkoa wa Kigoma Eng. Narcis
Choma, amebainisha changamoto zinazokabili mradi huo kuwa ni wizi wa mafuta na
vifaa vya ujenzi hali inayosababisha mradi kusuasua.
“Wananachi tambueni kuwa fedha hizi ni za kwenu
mnapohujumu vifaa vya ujenzi ni dhahiri mnajicheleweshea maendeleo na
kukwamisha fursa za kiuchumi katika wilaya yenu”, amesema Eng. Choma.
Kwa upande wake Mhandisi Mkazi Mekbib Tesfaye
anayesimamia mradi huo kutoka Kampuni ya DOCH Limited, amesema kuwa mradi huo
umefikia asilimia 24 ambapo kwa sasa kazi inayofanyika ni ujenzi wa madaraja mawili
na makalvati katika barabara hiyo.
Katika hatua nyingine, Waziri Prof. Mbarawa
ametembelea Chuo cha Mamlaka ya Hali ya Hewa Mkoani Kigoma na kuahidi uongozi
kuwa atazishughulikia haraka changamoto
kadhaa zinazokikabili chuo hicho ili
kuweka mazingira rafiki ya kujisomea kwa
wanafunzi wanaosomea taalauma hiyo.
“Nitahakikisha chuo hiki kinajengewa mabweni ya
wanafunzi pamoja na kuongeza gari kwa ajili ya shughuli mbalimbali
zinazofanyika hapa”, amefafanua Waziri Mbarawa.
Kaimu Mkuu wa Chuo hicho Peter Mlonganile wakati akisoma taaraifa ya chuo hicho kwa Waziri
huyo amesema kuwa licha ya kukabiliwa na changamoto hizo chuo hicho kinaendelea kutoa mafunzo hayo kwa
viwango vinavyotakiwa ikiwa ni
pamoja na kuzitatua changamoto ndogo ndogo zinazo kikabili chuo hicho.
Prof. Mbarawa yuko katika ziara ya kukagua miundombinu
ya barabara, reli, uwanja wa ndege, katika mkoa wa Kigoma ikiwa ni mkakati wa
Serikali wa kuboresha miundombinu hiyo na kuuwezesha mkoa kufanya biashara
kirahisi na mikoa mingine ya Tanzania na nchi za Congo DRC, Rwanda na Burundi.
Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini,
Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano.
Post A Comment: