WAZIRI wa Katiba na Sheria, Dk Harrison Mwakyembe amesema Serikali
imedhamiria kupunguza mashauri ya kesi ndogo ndogo ambayo yana watuhumiwa wengi
waliojazana magerezani ilhali mashauri yao yangeweza kumalizika kwa muda mfupi.
Aliyasema hayo jana Dar es Salaam
wakati alipokutana na kuzungumza na Jaji Mkuu wa Jimbo la Australia ya Kusini
nchini Australia, Chris Kourakis.
Alisema uwepo wa mashauri mengi
madogo ambayo watuhumiwa wake wanachukua nafasi kubwa kwenye magereza nchini,
serikali na mahakama imeona ni eneo lenye changamoto na hivyo linatafutiwa
ufumbuzi.
“Hili ni eneo moja ambalo mahakama
imeona linahitaji kufanyiwa kazi na liko kwenye maeneo ya ushirikiano baina ya
Tanzania na Australia Kusini, kwa sababu yakiangaliwa kwa ukaribu yatapunguza
msongamano kwenye magereza yetu na hata kuokoa gharama za kuwatunza,” alisema.
Akizungumzia maeneo ya ushirikiano
yaliyoafikiwa kati ya Jaji Kourakis, Jaji Mkuu wa Tanzania, Othman Chande na
Msajili Mkuu wa Mahakama, Katarina Revokati, Mwakyembe aliyataja kuwa ni
mafunzo na kuwajengea uwezo watumishi wa Mahakama, kuboresha mifumo ya Tehama
na kupitia upya Sheria ya Adhabu za Chini.
Akifafanua sheria hiyo, Katibu Mkuu
wa Wizara hiyo, Profesa Sifuni Mchome alisema inaweka kiwango cha chini cha
adhabu kwa makosa fulani ambacho hakimu haruhusiwi kutoa adhabu chini ya hapo
na kwa baadhi ya makosa.
Jaji Kaurakis alisema nchini Australia, Sheria hiyo ipo na
imeweka makosa machache ambayo jaji au hakimu haruhusiwi kutoa adhabu chini ya
hapo ili kutoa nafasi ya majadiliano na mtuhumiwa kwa lengo la kutaka mtuhumiwa
akubali na kukiri kosa kwa maana ya kujutia alichotenda.
Post A Comment: