Mkuu wa wilaya ya Hai,Gelasius Byakanwa akionesha sehemu ya nyaraka ambazo zinaonesha namna baadhi ya watumishi walivyoshiriki kufanya ubadhilifu wa fedha za madawati. Mkuu wa wilaya ya Hai,Gelasius By akanawa (katikati) akiwa na katibu tawala wa wilaya hiyo,Upendo Wela (kulia) pamoja na Mkurugenzi wa Halamshauri ya wilaya hiyo Yohana Sintoo (kushoto).
MKUU wa wilaya ya Hai, Gelasius
Byakanwa ametoa jukumu kwa mkurugenzi wa Halmashauri ya wilaya hiyo,Yohana
Sintoo la kuamua hatma yawatumishi wake watano wanaotajwa katika tuhuma za
ubadhilifu wa fedha wakati wa zoezi la utengenezaji wa madawati.
Akiwa ndio mamlaka ya nidhamu kwa
watumishi wa halmashauri hiyo,Mkurugenzi Sintoo ndiye mwenye maamuzi ya kuwasimamisha
kazi watumishi hao baada ya tume iliyoundwa na mkuu wa wilaya hiyo, Byakanwa
kumaliza kazi yake ya uchunguzi dhidi ya watumishi hao na kubaini mapungufu
kadhaa.
Akihitimisha taarifa yake wakati wa
kikao na watumishi wa halmashauri hiyo,Byakanwa aliagiza taasisi ya kuzuia na
kupambana na rushwa (TAKUKURU) kuchunguza na kuchukua hatua dhidi ya watumishi
hao akiwemo aliyekuwa kaimu Mkurugenzi ,Mhandisi Kweka.
“Mamlaka ya nidhamu ya watumishi wa
Halmashauri ni mkurugenzi pamoja na baraza la madiwani ,lakini mwajiri ni
ofisi ya katibu tawala mkoa ,Ofisi hizi mbili ndizo zinazoweza kukaa na
kuchukua hatua za kuzuia matukio au vitendo kama hivyo.”alisema Byakanwa.
“Niishauri ofisi ya Katibu tawala
mkoa wa Kilimanjaro pamoja na ofisi ya Mkurugenzi wa Halmashauri ya wilaya ya
Hai ambayo ndio mamlaka ya nidhamu kwa watumishi hao kupima kuhusu hatua
za kuchukua dhidi ya watumishi hawa”aliongeza Byakanwa.
Mkuu huyo wa wilaya alisema tuhuma
zinazowakabili watumishi hao ,majina yao tumeyahifadhi kwa sasa ni pamoja na
kupitisha barua ya malipo bila kujiridhisha kama kuna mkataba wa kutengeneza
madawati na kufanya malipo ya fremu za madawati badala ya madawati.
Tuhuma nyingine inaihusu timu ya
ukaguzi iliyokiri kukamilika kwa kazi bila ya kuonesha kama walipokea
madawati au walienda kukagua kazi ya mzabuni licha ya mzabuni kuomba
malipo ya fremu za madawati badala ya Madawati kamili.
Ofisi ya elimu msingi,ofisi ya
mkurugenzi,ofisi ya Mhasibu wa Halamshauri na kitengo cha manunuzi pia
zinatuhumiwa kushindwa kubaini nyaraka zilizowasilishwa na mzabuni endapo
zilikuwa ni kwa ajili ya fremu za Madawati badala ya Madawati kamili.
Katika kikao hicho kilichofanyika ukumbi wa
mikutano wa Halmashauri hiyo Byakanwa alisema kampuni iliyopewa zabuni ya
kutengeneza madawati ni ya Ujenzi na haijawahi kufanya kazi ya kutengeneza
madawati, kuwa na karakana wala vifaa vya uselemala .
Byakanwa
alisema kwa malipo yaliyofanyika Halmashauri ilipoteza zaidi ya sh Mil 12 huku
akishangazwa na hatua ya mmoja wa watumishi wanaotuhumiwa kuomba malipo badala
ya mzabuni.
Akionyesha namna watumishi hao walivyokiuka
taratibu Byakanwa alisema taarifa ya uchunguzi inaonyesha Halmashauri iliunda
timu ya ukaguzi ambayo katika cheti cha ukaguzi na mapokezi ya bidhaa
kinaonyesha bidhaa au madawati yalipelekwa ,Julai 16, 2016 ,siku 12 tangu siku
ya mkataba na mzabuni.
“Mmoja w wajumbe wa kamati hiyo ya ukaguzi
alikuwa ni mjumbe wa kamati ya kuratibu zoezi la Madawati ,alikuwa na jukumu la
kusambaza mbao kwa wazabuni na alikuwa anajua kuwa hajapeleka mbao za kutosha
kwa mzabuni ,katika maelezo yake mbele ya tume anakiri kuwa mzabuni hajamaliza
kazi kwa sababu Halmashauri haijampa mbao.”alisema Byakanwa.
Alisema mzabuni aliieleza tume kuwa
anadaiwa madawati 246 na halmashauri na kuwa amekamilisha kutegeneza madawati
154 na ueleza kua alishindwa kukamilisha kutokana na kukosa mbao kutoka
halmashauri.
“June 9,2016 malipo ya Sh Mil 19.2
yakalipwa kwa ajili ya fremu za madawati siyo Madawati.Vocha ya malipo ikasainiwa
na DT na kuandaliwa na mtumishi mwingine (jina tunalo) ikakamilisha
mchezo.”alisema Byakanwa.
Mkuu huyo wa wilaya alisema kufanya hivyo
ilikuwa ni kinyume cha taratibu za malipo kwa kuwa wahusika walipaswa
kujiridhisha na nyaraka walizokuwa wakitumia ,kwa nini mzabuni aliamua
kudanganya Halmashauri.
Byakanwa aliishauri ofisi ya Katibu tawala
mkoa wa Kilimanjaro pamoja na ofisi ya Mkurugenzi wa Halmashauri ya wilaya ya
Hai ambayo ndio mamlaka ya nidhamu kwa watumishi hao kupima kuhusu hatua
za kuchukua dhidi ya watumishi hao.
Kwa upande wake mkurugenzi wa Halmashauri
ya wilaya ya Hai,Yahana Sintoo alisema licha ya kwamba amefika wakati zoezi la
uchunguzi lina kamilika bado atafanyia kazi taarifa hizo kwa umakini mkubwa ili
kujiridhisha na utendajji kazi wa watumishi wa halmashauri hiyo.
|
Navigation
Post A Comment: