MTUMISHI WA UMMA ATAKAYESHINDWA KUWASILISHA TAARIFA ZAKE NA SIFA YA ELIMU ALIYONAYO HATAKUWA AMEJIFUKUZISHA KAZI IFIKAPO MACH 1

Share it:



Mtumishi wa Umma atakayeshindwa kuwasilisha cheti cha elimu na taaluma au “Index number” ya mtihani ili zihakikiwe na Baraza la Mitihani la Taifa (NECTA), itakapofika tarehe 1 Machi, 2017 atakua kajiondoa kazini mwenyewe.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais-Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. Angellah J. Kairuki (Mb) alibainisha hayo mwishoni mwa wiki wakati akifungua mkutano wa Watendaji Wakuu wa Wakala za Serikali jijini Dar es salaam.

“Watendaji Wakuu ninawaomba msimamie uhakiki wa vyeti ili watumishi wenu wafanye kazi kwa sifa stahiki” Waziri Kairuki alisisitiza.Aliongeza Serikali ilisitisha ajira mpya ili kupisha zoezi la kuondoa Watumishi hewa, zoezi ambalo limefika ukingoni na siku za karibuni ajira zitarudishwa.

Waziri Kairuki aliwataka Watendaji Wakuu kuweka mikakati ya kuepuka watumishi hewa na kusimamia kwa dhati kwasababu jambo hilo limeumiza na kupoteza rasilimalifedha nyingi za Serikali.

Alisema anatambua kuna Wakala zenye upungufu wa Watumishi hivyo zinaingia gharama kubwa za kuajiri wafanyakazi wa mikataba, hata hivyo alielekeza kila Mtendaji Mkuu ajiridhishe kwa kuandaa taarifa ya mahitaji halisi ya Watumishi.

Waziri Kairuki, pamoja na hilo alielekeza Wakala zenye Watumishi wa mikataba zifanye tathmini na kuhakiki kama kweli watumishi hao wanahitajika kwa kuwa eneo hilo ni moja ya maeneo yenye ajira za mashaka kwa baadhi ya Taasisi.

Waziri Kairuki aliongeza kuwa yapo malalamiko kuhusu suala la maadili na uwajibikaji yanayozigusa Wakala za Serikali. Aliainisha masuala hayo ni pamoja na Watumishi hewa, taarifa chafu za Watumishi, matumizi mabaya ya madaraka na rasilimali za Umma, kutosimamia ipasavyo utekelezaji wa mifumo ya utendaji kazi na wakati mwingine kutotekeleza majukumu ya msingi ya wakala.

Alifafanua kuwa amegundua kupitia taarifa mbalimbali kuwepo kwa  changamoto ya mawasiliano hafifu kati ya Wizara mama na Wakala zilizo chini yao ambapo taarifa kutoka katika Wakala hazichambuliwi inavyostahili na hata zinapochambuliwa na wizara mama, hazitoa mrejesho kwenda katika Wakala.

Awali, Katibu Mkuu Ofisi ya Rais-Utumishi Dkt. Laurean Ndumbaro alizitaka Wakala za Serikali kuimarisha eneo la ufuatiliaji na tathmini ili kuimarisha utendaji kazi na kuleta mabadiliko yanayotarajiwa na Watanzania.

 Alisema matarajio ya Serikali ya Awamu ya Tano ni kuhakikisha Wakala za Serikali zinapunguza utegemezi kwa Serikali kwa kujitegemea kimapato kutokana na vyanzo vyake vya ndani hasa kwa Wakala zinazoingiza mapato makubwa kutokana na huduma zinazotoa.

Serikali ilianzisha Wakala kwa lengo la kuzifanya vyombo vya kutekeleza majukumu kwa niaba ya Serikali kwa tija na ufanisi zaidi, pia kupunguza urasimu na hivyo kutoa huduma bora kwa wakati kwa wananchi.

Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano, Ofisi ya Rais-Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora.
Share it:

habari

Post A Comment: