Mkazi wa mtaa wa Mageuzi, kata ya Ngokolo, manispaa ya Shinyanga, Ibrahimu Daniel (42) amemuua mke wake, kwa kushindwa kuhifadhi vizuri kachumbari na kupika mboga isiyo na kiwango.
Aidha mauaji hayo yaliyofanyika kwa kumporomoshea kipigo yalifanyika kwa kuwa alipika chakula kingine wakati kilichobaki mchana kilikuwepo.
Aliyeuawa ni Stella Ibrahimu (39) na alipigwa baada ya mumewe Daniel kurudi nyumbani na kuuliza kachumbari ambayo alikula jana yake ndipo mtoto aliyekuwa akimlea Elizabeth Ibrahimu (13) alipomuonesha, lakini hakuridhika nayo na kuanza kuuliza maswali kwa nini haikuhifadhiwa vizuri.
Baadhi ya waandishi wa habari waliofika eneo la tukio walielezwa na mtoto wa marehemu, Daniel Ibrahimu (12) kuwa baba yake alipofika nyumbani saa moja usiku alimkuta yeye akiwa na Elizabeth ndipo alipoanza kumhoji Eliza akimuuliza kachumbari yake iko wapi.
Daniel alisema baada ya Eliza kumuonesha baba yake kachumbari hiyo aliyoila na kuibakisha Jumatatu wiki hii, aliiona imechacha na kuonekana na uchafu, ndipo alitoka nje na kuchukua fimbo anayoihifadhi juu ya nyumba na kutaka kuanza kumpiga lakini kabla ya kumpiga mtoto huyo alichoropoka na kukimbia nje.
Aliendelea kusimulia kuwa baada ya kukimbia na binti huyo, mama yake ambaye alikuwa kazini alifika nyumbani wakati huo mfarakano ukiendelea na alimkuta baba yao akifoka na baada ya kuuliza kuna nini, aliambiwa kwa nini hakupika mboga yenye kiwango na kwa nini alipika ugali mwingine wakati kulikuwa na ugali uliobaki mchana.
“Mama alifika na kuanza kunywa chai lakini baba aliendelea kufoka ndipo mama alimjibu kwa hasira ndipo alipomuuliza baba uliacha fedha ya matumizi ya kuweza kupika mboga yenye kiwango, alianza kumpiga baadaye alimpiga na kikombe na mateke akaanguka ndipo mimi nilikimbia kwa majirani kuwataarifu mama anapigwa, walikuja na kukuta mama ameanguka chini baba akiwa anamruka ruka,” alisema Daniel.
Baadhi ya majirani waliofika katika tukio hilo, Gloria Shija na Retisia Mashalah, walisema kwa nyakati tofauti kuwa, walikuta baba huyo amefunga mlango na walipomgongea afungue, alikataa na kusema kuwa kuna kazi kidogo anaifanya wasubiri, lakini baada ya kuchungulia dirishani walimuona anampuliza puani na masikioni huku akimmwagia maji ili azinduke, baada ya kuona hazinduki.
Shija alisema kuwa waliingia ndani na kumkuta akiwa amemkalisha chini huku akiwa ameinamisha shingo ambapo walimbeba na kumtoa nje, walijaribu kummwagia maji tena lakini ilishindikana ndipo walichukua uamuzi wa kumpeleka hospitalini walifika na kuanza kupimwa, lakini alionekana tayari alishafariki muda mrefu.
Kwa mujibu wa majirani, waliporudi nyumbani, mwanaume huyo alionekana kumtuma mara kwa mara mwanawe wa kiume na wakaingiwa na hofu na kutoa taarifa polisi ambapo walifika na kuwachukua watoto wawili; Daniel na Eliza kwa mahojiano.
Shangazi wa marehemu, Getruda Vitalis alisema ugomvi huo ulikuwa ukitokea mara kwa mara. Mwenyekiti wa mtaa wa Mageuzi, Emmanuel Sama alisema yeye alikuwa amelala nyumbani kwake aligongewa mlango na kuambiwa kuna tukio la mwanamke kupigwa na mume wake na ana hali mbaya ndipo aliamka na kwenda katika tukio.
Baada ya kuuliza aliambiwa chanzo ni kachumbari iliyobaki jana haikuhifadhiwa vizuri na mtoto waliokuwa wakimlea, Elizabeth.
Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga, Elias Mwita, alithibitisha na kueleza kuwa mtuhumiwa anashikiliwa na Polisi. Alisema uchunguzi wa awali katika mwili wa marehemu umeonesha kuwa na jeraha katikati ya kichwa na waliruhusu usafirishwe kesho wilayani Ngara, Kagera kwa maziko.
Post A Comment: