Naibu waziri wa nishati na madini Dr Medard Kalemani akiondoka eneo la mgodi baada ya kuona jitihada zinazoendelea
NAIBU waziri
wa Nishati na Madini Dk. Medard Kalemani ametembelea Mgodi wa RZ uliofukia
Watanzania 13 na raia mmoja wa Nchini China anayetambulika kwa jina la Meng
Juping na kusema kuwa serikali itaendelea kuweka nguvu ili kusaidia uokoaji.
Katika ziara
yake hiyo ya dharura Naibu Waziri huyo ametoa pole kwa niaba ya serikali kwa
uongozi wa Mkoa, Wananchi pamoja na Mgodi huo kukumbwa na tukio hilo.
Mara baada
ya kupokea taarifa ya maafa hayo, iliyosomwa na kamishina msaidizi wa madini
kanda ya ziwa victoria, Dk. Kalemani aliutaka uongozi wa Mkoa pamoja kamati ya
uokoaji kujikita zaidi kwenye shughuli ya uokojai na waachane na mambo mengine
ambayo yanaweza yakasababisha zoezi hilo liwe gumu.
‘’Ndugu
zangu mimi kwa niaba ya serikali kuu napenda nitoe pole kwa hiki kilichowakumba
Mkoa pamoja na Mgodi lakini napenda kuwaambia kuwa Kamati ya ulinzi na Usalama
pamoja natimu ya uokoaji mhakikishe mnasimamia vyema zoezi hili ili tuwaokoe
ndugu zetu ambao wamo humo ndani ya shimo,’’alisema Naibu waziri Kaleman.
‘’Kingine
niagize hapa hakikisheni mnatoboa shimo kwa kutumia drilling ili tupate mwanya
wa kuwapatia chakula ndugu zetu ambao wamefukiwa na udongo wakati juhudi za
kufukua zikiendelea ,’’aliongeza.
Akizungumza
na Maduka online mapema asubuhi ya leo kamishina msaidizi wa madini kanda ya ziwa
victoria Yahaya Samamba alisema kuwa kamati ya uokozi kwa kushirikiana kamati
ya ulinzi na usalama ya Mkoa wa Geita, ilibadilisha mfumo wa uokoaji kwa
kutumia wachimbaji wadogowadogo baada ya mashine za kisasa kufikia usawa mita
20 ambazo haziwezi kuhimili uzito.
‘’Mitambo
hii imekomea mita 20 tumeona tutumie wachimbaji wadogo ili twende sambaba na
uokoaji uliosalama..kwahiyo usiku wa jana (juzi) saa 5:00 kamili usiku
tulisitisha kutumia mashie yaani Magreda kutokana na usawa tuliofikia kuwa
laini,’’alisema Samamba.
Kwa upande
wake Mhandisi kutoka kampuni ya uchimbaji ya Busolwa Mine Eng. Nayompa wakati
akitoa mtazamo wake namna zoezi hilo linavyokuwa gumu alisema ramani
zinazotolewa na wachina ni za kubahatisha na hawana uhakika nazo ndizo sababu
zimechelewesha uokoaji na zoezi kuonekana halikamiliki kwa wepesi.
“Mimi
ninachokiona hapa wachina hawa ndugu zetu wachina wameshindwa kutupatia ramani ya
uhakika ndiyo maana tunabahatisha bahatisha tu..mwandishi hata wewe jana
ulikuwa shuhuda namna gari la kutoboa lilivyoshindwa kulenga kwenye shimo walipo ndugu zetu,’’alisema Eng. Nayompa.
Kwa upande
wake Mbunge wa jimbo la Busandwa ambako tukio hilo limetokea Lolensia Bukwimba
alisema haipaswi watu kunyosheana kidole kwa sasa wakati nguvu na jtighada
zikiendelea kufanywa.
Hata hivyo
Rais wa shirikisho wa vyama vya wachimbaji wa madini ,John Wambura
Bina,amepongeza juhudi ambazo zinafanyika kwa makapuni ya madini kujitolea
pamoja na serikali na wanaamini kuwa juhudi za uokoaji zinazoendelea zinaweza
kuzaa matunda.
Viongozi
mbalimbali wa serikali na chama jana walitembelea eneo la Mawemeru kuliko mgodi
wa RZ ambao unamilikiwa na wawekezaji wa Kichina huku leseni ya madini ikiwa ni
ya Mtanzania Ahamed Mbaraka.
Matumaini
kwa siku ya leo yanaonekana kwani hadi kufikia majira ya saa moja kamili watu
ambao wapo chini waligonga bomba kwa kuashiria kuwa wapo karibu na sehemu ya
kutokea.
IMEANDALIWA
NA MADUKA ONLINE
|
Post A Comment: