YANGA KUITAFUTA SIMBA

Share it:

Image result for KIKOSI CHA YANGA

Mabingwa watetezi wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Yanga, leo watajaribu kuitafuta Simba kwa kupunguza pengo la pointi dhidi ya vinara hao, kutoka nne hadi moja.

Simba inaongoza kwenye msimamo wa Ligi Kuu kwa pointi zao 44 baada ya kucheza mechi 18, wakifuatiwa na mabingwa watetezi, Yanga wenye pointi 40 za mechi 18 pia.

Na leo jioni Yanga watashuka Uwanja wa Majimaji mjini Songea kumenyana na wenyeji, Majimaji wakihitaji ushindi ili kujisogeza karibu kabisa na Simba.

Wachezaji watano wanakosekana kwenye kikosi hicho ambao ni beki Vincent Bossou ambaye yuko Gabon na timu yake ya Taifa ya Togo, mshambuliaji Mzimbabwe Donald Ngoma na viungo Wazambia Justin Zulu, Obrey Chirwa ambao wote ni majeruhi na Emmanuel Martin aliyekwenda kwenye msiba wa mdogo wake mkoani Tanga.

Lakini uzuri ni kwamba, Kocha Mzambia, George Lwandamina amebeba kikosi kipana kikiongozwa na makipa; Deo Munishi ‘Dida’, Ally Mustafa 'Barthez' na Benno Kakolanya, mabeki Hassan Kessy, Juma Abdul, Mwinyi Mngwali, Oscar Joshua, Andrew Vincent ‘Dante’, Pato Ngonyani, Nadir Haroub ‘Cannavaro’ na Kevin Yondan.

Viungo ni Said Juma ‘Makapu’, Thabani Kamusoko, Haruna Niyonzima, Juma Mahadhi, Deus Kaseke, Simon Msuva, Yussuf Mhilu, Geoffrey Mwashiuya na washambuliaji Amissi Tambwe, Malimi Busungu na Matheo Anthony.

Mbali na kuhitaji ushindi ili kujisogeza jirani na Simba, lakini pia Yanga wanatakiwa kushinda ili kurejesha furaha kwa mashabiki wao, baada ya timu hiyo kufanya vibaya kwenye michuano ya Kombe la Mapinduzi ikiwa ni pamoja na kufungwa na Simba.

Yanga ilipewa kipigo cha kukumbukwa cha mabao 4-0 na Azam FC katika mchezo wa mwisho wa Kundi B kabla ya kutolewa kwa penalti 4-2 na Simba baada ya sare ya 0-0 katika nusu fainali ya Kombe la Mapinduzi wiki iliyopita visiwani Zanzibar.

Na tangu hapo wapenzi wa Yanga wamekuwa wanyonge mbele ya wapinzani wao na kama si Simba kufungwa 1-0 na Azam FC katika fainali, bao pekee la Himid Mao hali ingekuwa mbaya zaidi kwa Wanajangwani.

Katika hatua nyingine kipa wa zamani wa Yanga, Said Mohammed Ndunda, anaweza kuisaidia timu yake hiyo baada ya kusema watawapunguza kasi Simba kesho katika Uwanja wa Jamhuri mjini Morogoro.

Mtibwa Sugar watakuwa wenyeji wa Simba Jumatano Uwanja wa Jamhuri mjini Morogoro katika mfululizo wa Ligi Kuu kuanzia kwenye mechi itakayopigwa saa 10: 00 jioni na Ndunda amesema watashinda mchezo huo.

“Naamini tutashinda mchezo huo, kikubwa tu ninawaomba mashabiki wa Mtibwa Sugar wa Morogoro na nje ya [mkoa huu] kwa ujumla waje kwa wingi Uwanja wa Jamhuri siku ya Jumatano kutushabikia mwanzo mwisho. Na wakija kwa wingi ni faraja kubwa kwetu,” alisema Nduda.

“Hatutowaangusha kabisa mashabiki wetu, kama wanavyojua mzunguko wa pili tumeanza vyema hatujapoteza mechi hata moja na tuna uhakika tutafanya vyema kwa kuwa tuna morali na tumejiandaa vizuri kuelekea mchezo huo, sisi tunapigana kwa pamoja hivyo lazima tupate matokeo mazuri” alisema Nduda.
Share it:

michezo

Post A Comment: