Shirika lisilo la kiserikali la Plan International Mkoani Geita limekabidhi kituo cha malezi na makuzi ya awali kwa watoto wadogo chenye thamani ya sh,milioni thelathini na nne laki nne na elfu tatu mia nne na tisini katika kata na kijiji cha Magenge wilayani hapa.
Akizungumza katika makabidhiano hayo na serikali ya kijiji,yaliyofanyika leo meneja wa Plan Mkoani humo Gratian Mushema Kweyamba,alisema kuwa lengo la ujenzi wa kituo hicho ni kumsaidia mtoto ambaye yupo chini ya umri wa miaka sifuri hadi miaka mitano (5) ambapo anaweza kujifunza mambo mbali mbali ya msingi.
“Tunaamini kuwa kituo hiki kitawasaidia watoto kupata elimu ya kujitambua wakiwa bado wadogo na ndio maana kauli mbiu yetu tunasema plan watoto kwanza, tunaamini kuwa mtoto akijengewa misingi mizuri pamoja na malenzi yaliyomema anaweza kuwa msaada kwa serikali na jamii inayomzunguka”Alisema Kweyamba.
Akielezea mafanikio ya ujenzi wa mradi huo,msimamizi wa kituo Bi,Lydia Wanjala,amefafanua kuwa tangua waanze ujenzi wamefanikiwa kwa kiasi kikubwa kutokana na jamii ambayo ipo eneo husika kutoa ushirikiano kwa kiasi kikubwa .
Akimwakilisha Mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya ,Afisa ustawi wa jamii ambaye ndiye alikuwa mgeni rasmi kwenye makabidhiano hayo Anderson Shimbi aliwashauri wanakijiji kuwa waangalizi wa mradi huo na kuutunza kwa uangalizi mkubwa zaidi.
“Ndugu zangu wanakijiji gharama iliyotolewa hapa ni kubwa sana hivyo tunatakiwa sisi wenyewe tuwe watu wa kwanza katika utunzaji wa mali hizi zilizopo kwenye kituo hiki”alisema Shimbi.
Diwani wa kata ya Magenge,Edward Misungwi,ametoa ahadi ya kuhakikisha wanakuwa walinzi wakubwa wa mradi huo na kwamba kwa mwananchi ambaye ataonekana kukiuka masharti yaliyowekwa hatua kali zitachukuliwa dhidi yake.
IMEANDALIWA NA MADUKA ONLINE.
Post A Comment: