TAARIFA YA WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA WAZEE NA WATOTO MHE. UMMY ALLY MWALIMU (MB) KWA VYOMBO VYA HABARI KUHUSU MAADHIMISHO YA SIKU YA WANAWAKE DUNIANI YA MACHI 8, MWAKA 2017 |
Nchi yetu kama zilivyo nchi nyingine wanachama wa Umoja wa Mataifa itaadhimisha Siku ya Wanawake Duniani ambayo kilele chake kitakuwa tarehe 8 Machi, 2017 na kwa mwaka huu itafanyika katika ngazi ya mkoa kwa kuzingatia amzingira ya mkoa husika.
Aidha Kaulimbiu ya maadhimisho ya mwaka 2017 ni “TANZANIA YA VIWANDA: WANAWAKE NI MSINGI WA MABADILIKO YA KIUCHUMI”. Kaulimbiu hii imetoholewa kutokana na Kaulimbiu ya Kipaumbele ya Umoja wa Mataifa mwaka huu katika Mkutano wa 61 wa Hali ya Wanawake Duniani (CSW) inayosema “Women Economic Empowerment in the Changing World of Work” ambayo tafsiri yake kwa lugha ya kiswahili ni “Uwezeshaji Wanawake: Kiuchumi Katika Dunia ya Mabadiliko ya Kazi”.
Kaulimbiu hii ya “Tanzania ya Viwanda: Wanawake ni Msingi wa Mabadiliko ya Kiuchumi” inalenga kuhamasisha jamii, Asasi za Kiraia, Sekta Binafsi, Taasisi za Serikali, Vyama vya Siasa, Wabia wa Maendeleo, mtu mmoja mmoja na wadau wengine hapa nchini Tanzania kuongeza wigo wa fursa za kiuchumi kwa wanawake ili kuwawezesha kushiriki na kunufaika na hatua za maendeleo katika kipindi hiki ambapo Tanzania inaelekea katika uchumi wa kati na wa viwanda.
Chimbuko la kuanzishwa kwa Siku ya Wanawake lilianza mwanzoni mwa miaka ya 1900 kufuatia maandamano ya wanawake wafanyakazi wa sekta ya viwanda nchini Marekani kupinga mazingira duni ya kazi. Waandamaji hao, walilalamikia ukosefu wa huduma za kijamii na kuwepo kwa vitendo vya unyanyasaji katika ajira ikiwemo wanawake kulipwa mshahara mdogo kwa kazi sawa ukilinganisha na wanaume.
Kwa kuzingatia hali hiyo, Umoja wa Mataifa baada kuanzishwa mwaka 1945 uliridhia kuwa tarehe 8 Machi kila mwaka iwe ni Siku ya Kimataifa ya Wanawake Duniani. Uamuzi wa Umoja wa Mataifa wa kuanzisha Siku ya Wanawake Duniani ulitokana na ukweli kwamba masuala ya haki, maendeleo na usawa wa wanawake yalihitaji msukumo maalumu na wa kipekee.
Lengo kuu la kuadhimisha Siku ya Wanawake Duniani ni kutoa fursa kwa jamii kupima utekelezaji wa maazimio, matamko, mikataba na itifaki mbalimbali za Kimataifa, kikanda na kitaifa zinazohusu masuala ya maendeleo ya jinsia na uwezeshaji wanawake. Hii ni pamoja na kuhakikisha kuwa haki za wanawake kiuchumi, kijamii, kiutamaduni na kisiasa zinapatikana na zinalindwa.
Kuadhimisha Siku ya Wanawake Duniani ni kuhamasisha jamii kuhusu umuhimu wa kutambua na kuthamini uwezo na mchango mkubwa wa wanawake katika kuleta maendeleo pamoja na kuelezea jitihada mbalimbali zilizofanywa na Serikali na wadau mbalimbali katika kuwajengea uwezo wa kiuchumi na kijamii ili waweze kushiriki kikamilifu katika kujiletea maendeleo yao, familia zao, jamii na Taifa kwa ujumla.
Aidha wanawake ni kundi kubwa na muhimu katika jamii (asilimia 51 ya Watanzania Wote) na kwamba hakuna maendeleo yeyote yanayoweza kufikiwa ikiwa kundi hili litaachwa nyuma.
Kwa mantiki hiyo, Serikali kwa kushirikiana na wadau imekuwa ikichukua hatua mbalimbali katika kuhakikisha wanawake wanashiriki na kunufaika na uchumi hasa katika kipindi hiki ambacho nchi yetu imejipanga kuelekea katika uchumi wa viwanda na kuwa nchi ya uchumi wa kati.
Taarifa ya Jukwaa la Uchumi Duniani kuhusu ‘Pengo la Jinsia ya Mwaka 2016’ inaonesha kuwa kutokana na jitihada zilizofanyika nchi yetu inashika nafasi ya 53 kati ya nchi 144 zinazofanya vizuri katika masuala ya jinsia Duniani.
Katika jitihada za kuwawezesha wanawake kiuchumi Serikali imeanzisha Mfuko wa Maendeleo ya Wanawake ambao unatoa mikopo yenye masharti nafuu kwa ajili ya kuwawezesha wanawake wajasiriamali wadogo kuanzisha na kuendeleza biashara, viwanda vidogo, kilimo pamoja na shughuli nyingine za kiuchumi.
Aidha kupitia Mfuko huo, Halmashauri zimehamasishwa kuchangia asilimia tano ya mapato yao ya ndani ambapo katika kipindi cha Julai hadi Disemba, 2016 kiasi cha shs. 4,102,808,513 kilitolewa kwa vikundi vya wanawake na vijana katika Halmashauri 101 kupitia utaratibu huu.
Benki ya Wanawake Tanzania pia ilitoa mikopo yenye thamani ya Shs 9,323,240,000/- kwa wajasiriamali 6,267 kati ya hao wanawake walikuwa 4,596. Hivyo, kiasi cha mikopo iliyotolewa imeongezeka kutoka Tshs. 112,473,600,000/- mwaka 2015 hadi kufikia Shs 121,796,840,000/- mwaka 2016.
Aidha, idadi ya wajasiriamali waliopata na kunufaika na mikopo inayotolewa na Benki ya Wanawake Tanzania iliongezeka kutoka wajasiriamali 79,983 mwaka 2015 hadi kufikia wajasiriamali 86,250 mwaka 2016 ambapo asilimia 73 ya wanufaika wa mikopo hiyo ni wanawake.
Kwa kutambua umuhimu wa ushiriki wa wanawake katika fursa mbalimbali za kiuchumi, Serikali imeratibu na kuzindua majukwaa ya uwezeshaji wanawake kiuchumi. Majukwaa haya yatatumika kama sehemu muhimu kwa wanawake wajasiriamali kukutana na kujadili fursa za kiuchumi pamoja na changamoto mbalimbali zinazowakabili na namna bora ya kukabiliana na changamoto hizo.
Aidha, sheria ya Utumishi wa Umma ya Mwaka 2002, (ilivyofanyiwa marekebisho mwaka 2007) imetoa fursa sawa za ajira kati ya wanawake na wanaume. Kwa mujibu wa Sheria hiyo, pale inapotokea mwanaume na mwanamke wanapata alama sawa wakati wa usaili, mwanamke anapewa kipaumbele kupata nafasi hiyo.
Sheria ya Kazi na Mahusiano Kazini (2004) imetoa fursa sawa kati ya wanawake na wanaume kuhusu haki zao za ajira, ikiwa ni pamoja na kuwepo kwa likizo ya uzazi kwa wanawake na wanaume.
Kwa kutambua elimu na mafunzo ni nyenzo muhimu katika kuhakikisha wanawake na wanaume wanashiriki na kunufaika ipasavyo na uchumi wa viwanda, Serikali imeendelea kuhakikisha kila mtanzania anapata elimu kama haki ya msingi.
Katika kuhakikisha kuwa mtoto wa kike na wa kiume wanapata haki ya elimu, Serikali inatekeleza sera ya Elimu bila malipo ambayo inatoa fursa ya Elimu ya Msingi na ya Sekondari na kuwahakikishia watoto elimu hiyo bila kujali tofauti za kiuchumi.
Sera hii imeleta mafanikio makubwa katika eneo hili ambapo takwimu zinaonesha kuwapo ongezeko la udahili kwa watoto wa kike na kiume
Pamoja na masuala yote yaliyotajwa hapo juu Kumekuwepo na ongezeko la ushiriki wa wanawake katika ngazi mbalimbali za maamuzi. Marekebisho ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1995 na ya mwaka 2005 yalifanywa na kuongeza idadi ya viti maalum kwa wanawake vilivyoongezwa hadi kufikia asilimia 30.
Katika kuhakikisha kuwa wanawake wanajengewa uwezo wa kisheria na kupata haki zao, sheria kadhaa zimetungwa na nyingine kufanyiwa marekebisho ikiwemo Sheria ya Makosa ya Kujamiiana yaani (SOSPA) ya mwaka 1998, ambayo imefanyiwa marekebisho na kuhuishwa kwenye Sheria ya Kanuni za Adhabu.
Sheria ya Ajira na Mahusiano kazini Na. 6 ya mwaka 2004 ambayo imetoa fursa sawa katika ajira na likizo ya Uzazi pamoja na Sheria ya Mtoto ya mwaka 2009; Sheria ya Ardhi na Sheria ya Ardhi ya Vijiji ya mwaka 1999, ambapo sheria hii inampa mwanamke haki ya kumiliki na kurithi ardhí sawa wanaume.
Pia, katika mwaka 2016/17 Bunge la Jamhuria ya Muungano limepitisha Sheria ya Msaada wa Sheria ya mwaka 2016 ambayo itasawadia wanawake hasa wenye kipato cha chini kupata haki zao za msingi.
Serikali inatambua kuwa ukatili dhidi ya wanawake bado ni tatizo kubwa ambalo linaathiri ushiriki wao katika shughuli za kiuchumi na kijamii.Katika kukabiliana na tatizo hilo, Serikali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali imeandaa Mpango Kazi wa Taifa wa Kutokomeza Ukatili Dhidi ya Wanawake na Watoto (2017/18 – 2021/22) ambao ulizinduliwa tarehe 13 Disemba, 2016.
IMETOLEWA NA WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA WAZEE NA WATOTO
Post A Comment: