JESHI LA MAGEREZA LAJITOSA KUJENGA VIWANDA VYA SUKARI NA VIATU

Share it:
Wakati Taifa likijielekeza kwenye ujenzi wa Tanzania ya viwanda na uchumi wa kati, Jeshi la Magereza nchini linatarajia kujenga upya kiwanda chake cha viatu cha Karanga na kuanzisha kiwanda kipya cha sukari katika Gereza la Mbigiri mkoani hapa.
 
Awali, Kiwanda cha Karanga kilichopo Wilaya ya Moshi mkoani Kilimanjaro kilishindwa kuendelezwa.
 
Ili kufanikisha hilo, tayari Shule ya Sekondari ya Bwawani inayomilikiwa na jeshi hilo imeanzisha mtalaa wa masomo ya sayansi ili kuandaa vijana wa kufanya kazi viwandani. 
Kamishna wa Utawala na Fedha wa Magereza, Gaston Sanga alisema mikakati hiyo inalenga kuunga mkono jitihada zinazofanywa na Serikali kutilia mkazo ukuaji wa uchumi kupitia viwanda.
 
Alisema taaluma inayotolewa shuleni hapo itakwenda sambamba na mahitaji ya wataalamu watakaotumika katika viwanda hivyo.
 
“Tumeona tuanzishe mchepuo wa masomo ya Sayansi yaani CBG (Kemia, Bailojia na Jiografia) kuanzia mwakani katika shule yetu ya Bwawani,” alisema kamishna huyo.
 
Alifafanua kuwa wameanzisha masomo hayo ili kupata wataalamu wengi watakaovisaidia viwanda vya jeshi na vingine vilivyopo nchini.
 
Kamishna Sanga alisema katika kuimarisha na kujenga upya kiwanda cha viatu na kile cha sukari, wanashirikiana na mifuko ya hifadhi za jamii ya PPF na NSSF.
 
Kuhusu Shule ya Sekondari ya Bwawani, alisema maendeleo ya kitaaluma yanategemea miundombinu ya madarasa, maabara, maktaba na ubora wa afya ya mwanafunzi.
 
Alipongeza jitihada zinazofanywa za kukamilisha kuendeleza miradi mbalimbali katika shule hiyo ili kuboresha maendeleo ya kitaaluma.
 
Pia, alisema ni vyema wazazi wawe mstari wa mbele kulipa ada kwa wakati ili kuwaruhusu wanafunzi kurudi shule mapema na walimu waweze kwenda sambamba na mitalaa iliyopo.
 
Kamishna Msaidizi wa Magereza, Emmanuel Lwinga ambaye pia ni mkuu wa sekondari ya Bwawani, alisema pamoja na jitihada za ujenzi wa nyumba mbili za walimu kwa mfumo wa kujitolea na madarasa mawili, bado wanakabiliwa na changamoto ya ukosefu wa jengo la utawala na nyumba za watumishi.
Share it:

habari

Post A Comment: