TPDC KUSAMBAZA GESI ASILIA KWA KUSHIRIKIANA NA SEKTA BINAFSI

Share it:




Na: Frank Shija – MAELEZO.
TPDC kwa kushirikiana na Sekta binafsi wanatarjia kutekeleza miradi mbalimbali ya usambazaji wa gesi asilian katika Mikoa ya Dar es Salaam, Pwani, Lindi, Mtwara na baadhi ya mikoa mingine itakayoidhinishwa.

Hayo yamebainishwa na Kiamu Mkurugenzi Mtendaji wa TPDC Mhandisi Kapuulya Musomba wakati akizungumza na waandishi wa habari Ofisini kwake jana  Jijini Dar es Salaam.

Mhandisi Musomba alisema kuwa miradi hiyo imeanza kwa kupitia upya taarifa ya awali ya upembuzi yakinifu wa mradi wa ujenzi wa mtandao wa bomba la kusambazia gesi asilia katika Jiji la Dar es Salaam, ambapo mnamo mwezi machi 22, 2017 TPDC ilikaribisha jumla ya makampuni 9 ambayo yalikidhi vigezo vya kimanunuzi kwa ajili ya kazi hiyo.
 
“Napenda kuutaarifu umma kuwa TPDC inatarajia kutekeleza miradi mbaimbali ya usambazaji wa gesi asilia katika mikoa ya Dar es Salaam, Bagamoyo na Mkuranga Mkoani Pwani, Lindi na Mtwara pamoja na baadhi ya mikoa mingine,” alisema Mhandisi Muyomba.
 
Aliongeza kuwa lengo la kupitia upya taarifa za awali ni kuboresha zaidi taarifa za kifedha, mahitaji ya kiufundi na utambuzi wa njia za kupitisha bomba na ugawaji wa kanda za usambazaji.
 
Aidha alisema kuwa ili kuharakisha usambazaji wa gesi, TPDC inakaribisha na kuhamasisha sekta binafsi kuwekeza katika uendelezaji wa miundombinu itakayowezesha usambazaji wa gesi asilia katika Jiji la Dar es Salaam mara tu mapitio ya upembuzi yakinifu utakapomalizika.
 
Mtandao huo unakadiriwa kuwa na urefu wa takribani kilomita 65 ambao utahudumia, kwa kuanzia, nyumba 30,000, viwanda na vituo vya kushindilia gesi asilia pamoja na vituo vya kujazia gesi hiyo.
 
Katika hatua nyingine Kaimu Mkurugenzi Mtendaji huyo alisema kuwa hadi sasa TPDC imefanikiwa kukiunganisha na mtandao wa gesi asilia Kiwanda kimoja cha kutengeneza Vigae cha Goodwill kilichopo Mkuranga, Mkoani Pwani huku likiendelea na majadiliano na viwanda vingine vitatu kwa ajili ya kuunganishwa na mtandao huo.
 
Kwa mujibu wa Sheria ya Mafuta ya Mwaka 2015 TPDC inatambuliwa kuwa Shirika rasmi la taifa linalojiendesha kibiashara, ambapo sheria hii inaipa mamlaka TPDC kuruhusu makampuni mbalimbali kuendesha shughuli za sekta, zitakazokuwa zainadhibitiwa kwa utaratibu maalum chini ya usimamizi wa Mdhibiti anayetoa leseni.

Share it:

habari

Post A Comment: