Kupitia kurasa zake za mitandao ya kijamii Nyalandu ameandika Ujumbe huu kama unavyosomeka hapo chini.
NIMEAMUA kujiuzulu NAFASI yangu ya Ujumbe wa Halmashauri Kuu ya Chama
Cha Mapinduzi CCM, pamoja na nafasi zote za Uongozi ndani ya Chama
kuanzia leo, Oktoba 30, 2017.
HALIKADHALIKA, asubuhi ya leo nimemwandikia Spika wa Bunge, Mh. Job
Ndugai, Mb., barua ya kujiuzulu nafasi yangu ya UBUNGE wa Jimbo la
Singida Kaskazini kupitia tiketi ya CCM, nafasi ambayo nimeitumikia kwa
vipindi vinne mfululizo tangu nilipochaguliwa kwa mara ya kwanza mnamo
mwaka 2000 hadi Sasa.
AIDHA, Nimechukua UAMZI huo kutokana na kutoridhishwa kwangu na mwenendo
wa hali ya Kisiasa nchini, ikiwa ni pamoja na ukiukwaji wa HAKI za
Kibinadamu, ongezeko la vitendo vya dhuluma wanavyofanyiwa baadhi ya
watanzania wenzetu, na kutokuwepo kwa mipaka ya wazi kati ya MIHIMILI ya
dola (Serikali, Bunge, na Mahakama) kunakofanya utendaji kazi wa
Kibunge wa Kutunga Sheria na wa Kuisimamia Serikali kutokuwa na uhuru
uliainishwa na kuwekwa bayana KIKATIBA.
VILEVILE, Naamini kwamba bila Tanzania kupata Katiba Mpya Sasa, hakuna
namna yeyote ya kuifanya mihimili ya dola isiingiliane na kuwepo kwa
ukomo wa wazi na kujitegemea kwa dhahiri kwa mihimili ya Serikali, Bunge
na mahakama ambayo ndio chimbuko la Uongozi Bora wa nchi, na kuonesha
kwa uwazi kuwa madaraka yote yatokana na wananchi wenyewe, na kwamba
Serikali ni ya Watu kwajili ya Watu.
MIMI Naondoka na kukiacha Chama Cha Mapinduzi CCM, nikiwa nimekitumikia
kuanzia ngazi ya Uenyekiti wa UVCCM Mkoa, Ujumbe wa Kamati za Siasa
Wilaya na Mkoa, Ujumbe wa Kamati ya Wabunge Wote wa CCM na Mjumbe wa
Halmashauri Kuu ya CCM TAIFA, kwani nimejiridhisha kuwa kwa mwenendo wa
hali ya kisiasa, kiuongozi na kiuchumi uliyopo Tanzania Sasa, CCM
imepoteza mwelekeo wake wa kuisimamia Serikali kama ilivyokuwa hapo
awali. AIDHA, Naamini kuwa, kama ilivyotokea kwa mihimili ya Bunge na
Mahakama kutokuwa na uhuru kamili, bila kuingiliwa kiutendaji kwa namna
Moja au nyigine, CCM nayo imekuwa Chini ya miguu ya dola badala ya chama
kushika hatamu na kuikosoa Serikali inapobidi kama yalivyokuwa maono ya
Baba wa TAIFA MWALIMU Julius Kambarage Nyerere.
HIVYOBASI, kwa dhamira yangu, na kwa uamuzi wangu mwenyewe, nikiwa na
haki ya KIKATIBA, natangaza KUKIHAMA Chama Cha Mapinduzi CCM leo hii, na
nitaomba IKIWAPENDEZA wanachama wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo
CHADEMA, basi waniruhusu kuingia MALANGONI mwao, niwe mwanachama, ili
kuungana na CHADEMA na watanzania wote wanaopenda kuleta mabadiliko ya
kisiasa na kiuchumi nchini kwa kupitia mfumo wa ki demokrasia na uhuru
wa mawazo.
VILEVILE, nimemua kujiuzulu KITI Cha Ubunge, Jimbo la Singida Kaskazini
kuruhusu kufanyika kwa UCHAGUZI mwingine ili wananchi wapate fursa ya
kuchagua ITIKADI wanayoona inawafaa kwa majira na nyakati hizi zenye
changamoto lukuki nchini Tanzania. Ni imani yangu, kamwe hayatakuwa ya
bure maneno haya, wala uamuzi huu niufanyao mbele ya Watanzania leo ili
kwamba, SOTE kama TAIFA tuingie kwenye mjadala wa kuijenga upya misingi
ya nchi yetu. Ni maombi yangu kwa MUNGU kuwa Haki itamalaki Tanzania.
Upendo, amani na mshikamano wa watu wa imani zote za dini, mitazamo
yote ya kiitikadi za Kisiasa, na makabila yote nchini uimarike.
Tushindane ki sera na kuruhusu tofauti za mawazo, lakini tubaki kama
ndugu, na TAIFA lililo imara na nchi yenye ADILI.
#MunguIbarikiTanzania.
Lazaro S. Nyalandu.
Post A Comment: