Kikosi cha Mbao FC cha mkoani Mwanza kina imani ya kutinga fainali ya Kombe la Shirikisho kwa kuing’oa na kuivua ubingwa Yanga.
Mbao FC wanajiamini kutokana na safu nzuri ya ushambuliaji, lakini wameandaa safu yao ya ulinzi kikamilifu kuwadhibiti Simon Msuva na Amissi Tambwe, kuhakikisha hawapati nafasi ya kufunga.
Mbao inatarajia kukutana na Yanga Jumapili katika Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza katika mchezo wa nusu fainali ya Kombe la FA ambapo hadi sasa ni timu nne tu ndizo zilizobakia.
Msemaji wa Mbao FC, Chrisant Malinzi, amesema kuwa, walikuwa na hamu kubwa ya kukutana na Yanga kwenye FA na kudai kuwa wameiandaa ipasavyo safu yao ya ulinzi kuhakikisha wanatoa upinzani mkubwa kwa Msuva na Tambwe ili wasipate nafasi ya kufunga kwa kuwa wanahitaji kutinga fainali.
“Tulianza mipango yetu siku nyingi ya kujiandaa katika michuano ya Kombe la FA na tulikuwa tukisubiria tu timu ya kupangwa nayo, tulikuwa na kiu ya kucheza na Yanga, kwani tupo tayari kwa mchezo huo na wala hatuhofii safu ya ushambuliaji ya Yanga kwani na sisi tuna safu nzuri ya ulinzi ya kuweza kuwazuia Msuva na Tambwe, tumejipanga vyema kuhakikisha tunapata nafasi ya kuingia fainali.
“Kikosi chetu kipo vizuri na hadi tunafikia hapa ni juhudi za wachezaji hivyo nina imani tutafanikiwa kufanya vyema na hatimaye kuingia fainali kwani lengo letu ni kuona tunafanikiwa kutwaa taji ili kuwakilisha nchi kimataifa,” alisema Malinzi.
Post A Comment: