Inaweza kuonekana ni kitu cha kawaida lakini kuwa na furaha ya kweli na ya kudumu ni kitu ambacho kinatafutwa sana na watu wengi. Ndio maana ukichunguza, harakati nyingi za kutafuta maisha zinalenga hasa kupata furaha.
Hata hivyo pamoja na watu wengi kuitafuta furaha sana, lakini bado wengi pia wanaendelea kugubikwa na huzuni nikiwa na maana ni watu ambao wanaishi maisha hayana furaha sana kwa sehemu kubwa.
Je, hebu tujiulize ni mambo gani ambayo yanasababisha mtu mmoja akawa na furaha au mwingine akaikosa furaha? Majibu ya maswali haya utayapata kwenye makala haya. Kikubwa fuatana nasi tuweze kujifunza pamoja.
1. Kufanya kazi usiyoipenda.
Ipo asilima kubwa sana ya watu ambao wanafanya kazi ambazo mara nyingi wanakuwa hawazipendi sana. Kwa lugha rahisi wanakuwa ni watu wanafanya kazi ambazo hawazifurahii, kikubwa kwao inakuwa ni kutaka kuingiza kipato tu basi.
Kama unafanya kazi ya namna hii ambayo huifurahii, lakini lengo lako ni kuingiza kipato basi elewa unabeba moja ya kitu ambacho kinakuzuia kupata furaha katika maisha yako kwa namna moja au nyingine.
Watu wote wenye mafanikio wanafanya vile vitu ambavyo wanavipenda kutoka moyoni mwao. Kama hufanyi kitu unachokipenda, leo hii ukianza kufanya kitu ambacho unakipenda, uwe na uhakika utaanza kujenga furaha yako.
2. Kujilinganisha na wengine.
Ni tabia ya wengi wetu tangu tukiwa watoto wadogo kutaka kujilinganisha na watu wengine. Kwa bahati mbaya tabia hii imekua ikikua hadi kuweza kufikia ukubwani na kwa wengi wetu tena tumekuwa tukiindeleza pasipo hata kujua.
Mara nyingi tumekuwa tukijilinganisha katika vipato vyetu, tumekuwa tukijilinganisha katika mavazi na mambo mengine chungu nzima. Hivyo, kutokana na kujilinganisha huko sana imekuwa ikipelekea sisi kukosa furaha.
Kikawaida huwezi kuwa na furaha kama kila wakati unajilinganisha na wengine. Maisha na furaha yako inabaki kuwa yako kama kweli unaishi wewe kama wewe. Kujilinganisha na wegine ni sawa na kutengeneza mazingira ya kupoteza furaha yako moja kwa moja.
3. Kuogopa mambo mengi.
Ni asili ya binadamu kuwa na hali fulani ya woga. Kuna wakati tunakuwa tunaogopa mambo yanayotudhuru au kuna wakati tunakuwa tunaogopa kujiingiza katika jambo fulani , mathalani hata uthubutu wa kufanya kitu fulani.
Sasa inapotokea unakuwa ni mtu wa kuogopa sana mambo mengi na kila wakati, hiyo inakuwa ni changamoto mojawapo ambayo inakuzuia moja kwa moja wewe kuweza kupata furaha ya kweli.
Furaha ya kweli mara nyingi inapatikana hasa kwa wewe unapokuwa huru na mambo yako.
Unapokuwa huru huna hofu ya mambo mengi na kuishi kwa kujiamini, hapo ndipo unakuwa na furaha ya kweli.
4. Kuishi wakati uliopita.
Kuna watu ambao wengi wetu badala ya kuishi sasa, hujikuta ni watu wa kuishi kwa kukumbuka sana matukio mengi yaliyopita. Kama unaishi hivi kwa kukumbuka mambo mengi yaliyopita na ambayo yalikuumiza kwa namna moja au nyingine uwe na uhakika, furaha yako utaipoteza.
Kujenga furaha ya kweli unatakiwa kuishi sasa na wala si kesho. Fanya mambo yako kwa kuzingatia sana sasa. Watu wngi wenye mafanikio na furaha ya kweli wanaishi sasa na kusahau mambo mengi yaliyopita.
Kumbuka wewe ndiye unayewajibika na kutengeneza furaha ya kweli katika maisha yako. Zingatia mambo hayo yanayokuzuia kupata furaha ya kweli.
Navigation
Post A Comment: