KILA ifikapo Mei 3 ya kila mwaka wanahabari na wadau wa vyombo vya habari ulimwenguni huadhimisha Siku ya Uhuru wa Vyombo vya Habari Duniani. Maadhimisho ya mwaka huu (2017) kitaifa nchini Tanzania yalifanyika mkoani Mwanza na kushirikisha wanataaluma ya habari na wadau anuai wa vyombo vya habari.
Miongoni mwa hoja zilizoteka mijadala katika maadhimisho ya Siku ya Uhuru wa Vyombo vya Habari Duniani kwa mwaka 2017 jijini Mwanza ni suala zima la usalama wa wanahabari wanapokuwa wakitekeleza wajibu wao pamoja na uwepo wa mafunzo anuai ya mara kwa mara kwa wanahabari kuwanoa zaidi.
Chama cha Wanahabari Wanawake Tanzania (TAMWA), ni miongoni mwa taasisi wadau waliofanikisha maadhimisho ya Siku ya Uhuru wa Vyombo vya Habari Duniani mwaka 2017 kitaifa yaliofanyika mkoani Mwanza. Bi. Valerie Msoka ni Mwanachama wa TAMWA, akizungumza katika maadhimisho ya mwaka huu kuwasilisha ujumbe wa chama hicho kwa wadau wa habari.
Anasema TAMWA imejitahidi katika kuwanoa wanahabari ili kuhakikisha wanabobea kwenye maeneo mbalimbali ya uandishi wa habari huku lengo likiwa kuwajengea uwezo zaidi. Bi. Msoka ambaye pia aliwahi kuwa Mkurugenzi Mtendaji wa TAMWA hapo nyuma kabla ya uongoziwa wa Mkurugenzi wa sasa wa chama hicho, Edda Sanga anabainisha wamekuwa mstari wa mbele katika kuchangia weledi na ubobezi wa wanahabari hasa katika uandishi wa habari za ukatili kwa jamii.
Anasema tamwa katika mpango mkakati wake wa kuelimisha jamii kuondokana na vitendo vya ukatili wa kijinsia hasa kwa wanawake na watoto kwa kipindi cha mwaka 2015 na 2016 imeelimisha idadi kubwa ya wanahabari kwenye ubobezi wa uandishi wa habari za ukatili wa kijinsia eneo ambalo limekuwa likionekana kupwaya kiuandishi.
Wanahabari kutoka vyombo mbalimbali vya habari nchini zaidi ya wanahabari 2350 na wahariri 120 walijengewa uwezo wa jinsia ya kuandika habari za ukatili wa kijinsia zenye kuleta mabadiliko katika jamii ambapo kwa sasa vitendo hivyo vinatolewa taarifa kwa usahihi ukilinganisha na awali.
Anasema waandishi hao baada ya kupata mafunzo hayo wamekuwa wakitumia ujuzi huo kuandika na kuibua habari za vitendo vya ukatili wa kijinsia jambo ambalo limesaidia baadhi ya maeneo mamlaka husika kuchukua hatua juu ya vitendo hivyo, hali ambayo imekuwa ikisaidia kupungua kiasi fulani kwa vitendo hivyo kwenye jamii ukilinganisha na hapo awali.
Post A Comment: