KESI YA CUF INAYOHOJI UHALALI WA BODI YA WADHAMINI YA LIPUMBA KUSIKILIZWA MACHI 27

Share it:
Na Regina Mkonde
 Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam imepanga kusikiliza mashauri mawili Namba 557 na 558/2017 yaliyofunguliwa mahakamani hapo na Wajumbe wa Baraza Kuu la Uongozi la Taifa la CUF dhidi ya Wakala wa Usajili, Udhamini na Ufilisi-RITA.

Kesi hizo zinahoji uhalali wa wajumbe wa Bodi ya Udhamini CUF walioteuliwa na Mwenyekiti wa chama hicho anayetambuliwa na Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa, Prof. Ibrahim Lipumba, zitasikilizwa mbele ya Jaji wa Mahakama Kuu, Zainab Goronya Muruke.

Taarifa hiyo imetolewa jana kwa vyombo vya habari na Naibu Mkurugenzi wa Habari, Uenezi na Mahusiano na UmMa CUF, Mbarala Maharagande.

Pia, Maharagande alisema Mahakama Kuu imepanga kusikiliza mfululizo kesi za CUF ambazo jana ziliahirishwa kusikilizwa kutokana na Jaji anayesimamia kesi hizo, Wilfred Ndyansobera kupata na udhuru.

Maharagande amesema kesi hizo ambazo ni Na. 28, 68, na 80 za mwaka 2017 zinazohusu Wizi wa fedha za Ruzuku ya CUF, Na. 21/2017 inayohusu Wabunge 19 wa CUF dhidi ya Lipumba na wenzake pamoja na kesi Na. 13/2017 iliyofunguliwa na Ally Salehe dhidi ya RITA, zitaanza kusikilizwa kuanzia Aprili 16, 17 na 18 mwaka huu.

“Shauri la Msingi Namba 23/2017 kuhusu Uhalali wa Uenyekiti wa Lipumba ambalo lilikuwa Mahakama ya Rufaa Tayari lisharejeshwa Mahakama Kuu na limepangwa kutajwa Tarehe Aprili 19, 2018 mbele ya Jaji Ignus Paul Kitusi,” amesema.
Share it:

habari

Post A Comment: