Mzee Yusufu Bangili ambaye ni mkazi wa mtaa wa Nyakabale akielezea namna ambavyo wameendelea kushuhudia Polisi Jamii wakiwapiga wananchi wa mitaa ya Manga na Nyakabale. |
Mdogo wa marehemu Bw, Majaliwa Shaban,akizungumza na waandishi wa habari namna ambavyo kaka yake alivyoweza kukutwa na umauti. |
Nyumbani kwa marehemu Zacharia Shaban,baadhi ya wananchi wakiwa kwenye hali ya maombolezo. |
Mke wa Marehemu,Zacharia Majaliwa ,Bi Leah Joseph akiwa kwenye hali ya maombolezo pamoja na watoto wake wanne ambao wameachwa na Baba yao. |
Wananchi wakiwa wamevunja kibanda kwenye familia ya mwenyekiti wa mtaa wa Nyakabale. |
Baadhi ya wananchi wa mtaa wa Nyakabale wakitoka kwa mwenyekiti wa mtaa huo baada ya kuwa wameupeleka Mwili wa Marehemu. |
Na,Joel Maduka,Geita.
Baadhi ya Wananchi wa
mtaa Nyakabale Kata ya Mgusu kwenye
halmashauri ya mji wa Geita ,wamegoma kuuzika mwili wa Bw ,Zacharia Shaban na
kuutelekeza nyumbani kwa Mwenyekiti wa mtaa huo, Bw Elias Ndarawa kwa madai kuwa
ameshindwa kutoa ushirikiano na kutoshughulikia tukio la kupigwa mkazi huyo na polisi jamii hadi
kufariki.
Mke wa marehemu Bi Leah
Joseph ,alisema mume wake alikwenda kufanya shughuli za utafutaji na kwamba
ndani ya siku saba hakuwepo Nyumbani na aliporudi alikuja akiwa na majeraha
huku kichwa chake kikiwa kimevimba huku akilalamika kuwa ameumizwa na Polisi
jamii na kudai kuwa hawezi kupona kutokana na hali aliyokuwa nayo.
Mdogo wa marehemu Bw, Majaliwa
Shaban, alisema tukio hilo lilitokea siku ya jumatatu kwani marehemu alikwenda
kuokota mabaki ya mawe ya dhahabu maarufu kwa jina la (MAGWANGALA) kwenye
maeneo ya mgodi wa dhahabu wa Geita(GGM) na alikamatwa na kufikishwa polisi
ambapo huko amekaa siku sita na baada ya kurudi nyumbani ndipo hali yake ilizidi
kuwa mbaya.
Majaliwa aliendelea
kusema kuwa walimpeleka hospitali na siku ya Jumamosi Machi 10, 2018 alipoteza
maisha akiwa hospitalini kabla ya kupatiwa matibabu na kwamba baada ya kifo
walijaribu kumtafuta Mwenyekiti na Mtendaji ambao hata hivyo hawakupokea simu hali
iliyosababisha wananchi kubeba mwili na kuupeleka kwa Mwenyekiti.
Bw Mussa Mashauri
ambaye ni mkazi wa mtaa huo alisema hawako tayari kuzika hadi serikali itakapotoa
kauli kuhusu hatma ya maisha yao na polisi jamii kutokana na namna ambavyo
wameendelea kuwapiga na kuwajeruhi.
“Polisi jamii badala ya
kutulinda wamekuwa wakitupiga hadi kufikia hatua ya kutudhuru na hilo Mwenyekiti
analijua na hajawahi kuingilia kati na kutusaidia na sisi hatujakataa kumstiri
ndugu yetu, tunachotaka ni muafaka wa kutuambia ni lini wataacha Polisi jamii
kutupiga”Alisema Mussa.
Hata Hivyo mtandao huu
ulipotaka kuzungumza na Mwenyekiti wa mtaa huo, Bw Elias Ndarawa aligoma
kuzungumzia tukio hilo kwa madai kuwa anaisubiria serikali ndio yenye atoe
kauli yake.
Aidha diwani wa Kata ya
Mgusu Bw Pastory Ruhusa alifika kwenye eneo hilo na kusema kuwa hatua ya
wananchi kuutelekeza mwili wa marehemu kwa mwenyekiti sio suala zuri huku
akiwataka wananchi kuwa na subira hata kama kuna tatizo na kuachana na
tabia ya kujichukulia sheria Mkononi.
Kutokana na madai hayo
Jana,Machi 11,2018 wananchi walivamia kituo cha Polisi Jamii ambacho kipo mtaa
wa Manga na kuvuruga miundo mbinu mbali mbali na kisha kukichoma moto kwenye
baadhi ya maeneo.
Post A Comment: