MOTO WATEKETEZA MADUKA NANE

Share it:








Na Stella Kalinga, Simiyu
Moto ambao hadi sasa chanzo chake hakijafahamika umeteketeza maduka nane , stoo pamoja na mali za wafanyabiashara  ambazo thamani yake haijafahamika, katika Mji mdogo wa Lamadi wilaya ya Busega Mkoani Simiyu , usiku wa tarehe 02 Juni.

Akizungumzia jinsi moto huo ulivyoanza mmoja wa wakazi wa Lamadi aliyeshuhudia tukio hilo, Bw. John Balele amesema moto ulianza kuwaka katika moja ya chumba cha duka majira ya saa mbili usiku na baadaye ukaanza kusambaa katika vyumba vingine lakini hawakuweza kufahamu chanzo chake maana vyumba vyote vilikuwa vimefungwa.

“Huu moto umetokea majira ya saa mbili hivi tulivyouona tukapiga simu polisi, askari polisi wakaja na askari wa zimamoto, Zimamoto wamejitahidi kuwahi kufika na wametusaidia sana kutuelekeza namna ya kukabiliana na moto huu tukafanikiwa kuuzima na kuokoa baadhi ya mali  japo mali nyingi zimeteketea lakini hakuna mtu aliyedhurika; binafsi nawashukuru sana wananchi wenzangu wa Lamadi kwa moyo wao wa kujitolea” alisema John Balele.

Diwani wa kata ya Lamadi, Mhe. Laurent Bija amewashukuru wananchi kwa namna walivyojitoa kushirikiana na jeshi la polisi na kikosi cha Zimamoto na uokoaji katika kuukabili moto huo na kulinda baadhi ya mali zilizookolewa kwa uaminifu .

Aidha, Diwani huyo ametoa pole kwa wafanyabiashara ambao mali zao zimeteketea na akatoa wito kwa wafanyabiashara wote katika Kata hiyo kuwa na vifaa vya kuzimia moto katika maeneo yao ya biashara, ili viweze kuwasaidia katika hatua za awali za kukabiliana na moto pindi unapotokea.

Akizungumza wananchi wa Lamadi waliojitokeza kuzima moto huo wakishirikiana na Jeshi la Zimamoto na Uokoaji na Jeshi la Polisi Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka amewapa pole wafanyabiashara ambao wamepoteza mali zao katika ajali hiyo ya moto na akawashukuru wananchi wa Lamadi kwa ushirikiano na uaminifu waliounesha wakati wa kuzima moto huo.

Mtaka amesema kwa kuwa chanzo cha moto huo hakijafahamika Serikali kupitia TANESCO na Zimamoto itaendelea kutafuta na kubaini chanzo na tarehe 03 Juni, 2018 Serikali itafanya tathmini kujua madhara yaliyosababishwa na moto huo.
“ Nawapa pole wananchi wa Lamadi bado hatujajua chanzo hasa, wenzetu wa TANESCO na Zimamoto watatusaidia kujua chanzo, kuhusu madhara kwa kuwa sasa ni usiku kesho Serikali itafanya tathmini ili na sisi tuone namna ya kuzungumza na wenzetu wa benki na kuona busara gani itumike kuwasaidia wafanyabiashara waliokopa namna ya kurejesha, wakati wanajipanga upya” alisema
Mkuu huyo wa Mkoa pia ametoa wito kwa Taasisi za Bima hapa nchini kupanua wigo na kuwafikia wafanyabiashara na kuona namna sahihi ya kuwa msaada kwao pale wanapokutana na majanga yasiyoepukika yakiwemo ya moto, huku akisisitiza wafanyabiashara kuchukua tahadhari ya moto ikiwa ni pamoja na kuhakikisha vifaa vyote vya umeme vimezimwa wanapofunga biashara zao.  
Katika hatua nyingine  ametoa wito kwa Jeshi la Zimamoto kuendelea kutoa elimu ya majanga ya moto hasa kwenye maeneo ya masoko ili waweze kuchukua tahadhari ya moto na akawataka wale wanaojenga majengo ya biashara kupata ushauri wa kitaalam juu ya ujenzi wa majengo yao


Kamanda wa Zimamoto Mkoa wa Simiyu, Gervas Fungamali amesema Jeshi la polisi litaendelea kutoa elimu  kwa wananchi hususani juu ya umuhimu wa kuwa na vifaa vya kuzimia moto na kuchukua tahadhari ya moto katika maeneo yao.
Share it:

habari

Post A Comment: